MLANGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umefunguliwa kwa Ester Matiko, Ester Bulaya, Halima Mdee na wengine waliofukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujiunga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wito wa wanasiasa hao waliokuwa wanachama wa Chadema kujiunga na CCM, umetolewa na Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM tarehe 29 Novemba 2020 wakati wakati akifungua semina ya wajumbe wa sekretarieti ya taifa ya halmashauri kuu na kamati ya utekelezaji wa jumuiya za chama hicho.
“Tunawakaribisha.., milango iko wazi” amesema Dk. Bashiru huku akisisitiza “chama cha siasa kinachogharamiwa na watu wa nje, hicho sio chama.”
Dk. Bashiru ametoa kauli hiyo ikiwa ni baada ya Bulaya na wenzake kutimuliwa uanachama wa Chadema kutokana na kukiuka misingi ya chama hicho, kwa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu.

Chadema kupitia John Mnyika, katibu mkuu wa chama hicho alipokutana na waandishi wa habari wiki iliyopita alieleza, wanachama hao 19 walioapishwa kuwa wabunge, walijiteua wenyewe baada ya kuasi msimamo wa Chadema wa kutotambua matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Mbali na Matiko, Bulaya na Mdee kufukuzwa Chadema, wengine ni Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje; Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega; Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga; Naibu Katibu Mkuu Bawacha, Jesca Kishoa na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.
Yupo pia Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.
Leave a comment