June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Matibabu ya moyo kunufaisha watoto 60%

Dk. Narva Gershan (kulia) akimpima mtoto mwenye ugonjwa wa moyo

Spread the love

ASILIMIA 60 ya watoto wanaokosa huduma ya matibabu ya moyo wanatarajia kunufaika na mpango wa matibabu hayo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mpango huo ni wa “kuwatambua watoto wenye ugojwa wa moyo ambao wanahitaji tiba ya upasuaji ili kuwafanyia vipimo vya awali na kuwasafirisha kwenda nchini Israeli kwa matibabu”

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Dk. Namala Mkopi- Makamu wa Rais, Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania, amesema “zoezi hili limeanza jana na litamalizika 25 Machi mwaka huu. Linafanyika kwenye kitengo cha magojwa ya moyo Muhimbili”.

“Uwezo wa wizara kwa sasa ni kuhudumia asilimia 40 ya watoto. Asilimia 60 wanasubili kupata huduma hii. Takribani asilimia 25 ya waliokuwa wakisubili huduma mwaka 2012/2014 walifariki. Vifo vitaendelea kutokea iwapo hawatapatiwa huduma hii haraka,” amesema Mkopi.

Mkopi amesema mpango huo unaratibiwa na Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania, asasi ya kiraia ya Save a Child Heart (SACH) kutoka Israel na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Katika mchakato huu SACH itagharamia matibabu, malazi na chakula kwa watoto watakaopelekwa Israel. Muhimbili itatumia wataalam wake na vifaa vilivyopo na kuhakikisha upimaji wa watoto na matibabu ya awali kabla ya kusafiri kwenda Israel yanapatikana,” amesema Mkopi.

Aidha, amesema Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania kimejikita zaidi kwenye kuratibu mchakato na kuwashirikisha wadau wengine ili kuweza kupata nauli ya kuwasafirisha watoto kwenda Israel ambapo tiketi kwa mtoto mmoja inaghalimu sh. 2,700,000.

Naye Dk. Narva Gershan kutoka SACH amesema “kila mtoto ana haki ya kuishi katika mazingira mazuri. Hivyo kazi yetu ni kuhakikisha tunawapa matibabu na kuwarejesha katika nchi zao na kuwafuatilia. Matibabu yetu yanawapa fursa ya kutimiza ndoto zao”.

Mtoto Nasra Khamis (12) mkazi wa mji mpya kutoka mkoani Arusha ameliambia MwanaHALISI Online kuwa, “mama yangu amenileta hapa tangu jana. Mwaka 2013 niligundulika nina tatizo la moyo. Niliacha shule nikiwa darasa la sita mwaka 2012 kwa sababu ya kuumwa. Naomba watu wanisaidie nitibiwe, nirudi shule, nisome ili niwe rubani”.

Takwimu zinaonesha kati ya watoto 1.7 milioni wanaozaliwa kwa mwaka nchini, watoto 13,600 wanazaliwa na magojwa ya moyo. Kati yao asilimia 25 wanahitaji kufanyiwa upasuaji.

error: Content is protected !!