August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mateso Zanzibar ‘yamponza’ Kubenea

Spread the love

MWANDISHI mahiri wa habari za uchunguzi nchini, Saed Kubenea, amehojiwa na makachero wa jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Anatuhumiwa kuandika makala ya uchochezi kuhusu mgogoro wa kisiasa Visiwani, anaandika Faki Sosi.

Kubenea aliandika makala hiyo katika gazeti la MwanaHALISI linalochapishwa kila siku ya Jumatatu.

Makala inayodaiwa na watawaka kuwa ya kichochezi ilibeba kichwa cha maneno: “Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?” Ilichapishwa katika toleo la Julai 25 hadi 31 mwaka huu.

Makala katika MwanaHALISI imeeleza malalamiko ya dhidi ya jinsi jeshi polisi kisiwani Pemba kuwa, linawabambikiza kesi wananchi, kuwapiga na kuwatesa kwa madai ya kuipinga serikali iliyopo madarakani.

Kubenea alifika katika kituo cha Polisi Kati, majira ya saa saba na robo mchana (13:15) wa Jumatatu, 15 Agosti akiwa ameongozana na wanasheria wake, Tundu Lissu na Frederick Kihwelo.

Alihojiwa kwa zaidi ya saa mbili; baada ya kutoka kituoni alizuiwa kuongea na waandishi wa habari waliokuwapo eneo hilo.

Hata hivyo, Kubenea ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), inayochapisha magazeti ya MwanaHALISI na MSETO amemueleza mwandishi wa habari hizi kuwa, “pale hakuna kosa lolote lililotendeka. Kilichofanyika kinalenga vitisho dhidi ya waandishi.”

Amesema, “hakuna wa kunyamaza. Hakuna kurudi nyuma kwa kuwa yote niliyoandika, yamekuwa yakisemwa ndani ya Bunge; nje ya Bunge na kwenye vyombo vya habari vya ndani na vile vya kimataifa.”

“Madai haya yameelezwa na wabunge bungeni. Wamemtuhumu hata naibu mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Visiwani, Salum Msangi. Kuna mashitaka yamepelekwa mahakama ya uhalifu dhidi ya binadamu ya The Hugue. Nakuambia hivi, hakuna kuogopa. Nitaandika na sitaacha,” ameeleza Kubenea.

Mbali na kuwa mwandishi wa habari na mkurugenzi wa HHP Limited, Kubenea pia ni mbunge wa jimbo la uchaguzi la Ubungo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Naye Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema amewambia waandishi wa habari kuwa Kubenea amehojiwa kwa madai ya uchochezi lakini alichokiandika ni hali halisi ya Zanzibar hususani kisiwani Pemba.

Amesema, “Kubenea amechiwa kwa dhamana na ameamriwa kurudi tena kituoni hapo tarehe 18 Agosti. Ni vema kesi hii ikaenda mahakamani ili niweze kupata nafasi ya kuwaumbua hawa watawala.”

Kubenea aliandika makala hiyo baada ya kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba kufuatilia kile alichokitaja kama “mateso, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi.”

Miongoni mwa wahanga waliozungumza na mwandishi huyo wa habari, ni Hijja Hassani aliyetangazwa kuwa ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba, kabla ya Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi huo na matokeo yake.

Kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huru na haki Visiwani, ndiyo chanzo cha mgogoro wa kisiasa ulioikumba Zanzibar.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, hatua ya polisi kumhoji Kubenea na baadaye kumfikisha mahakamani, kutaibua upya mgogoro huo wa kisiasa.

error: Content is protected !!