Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Matatizo sekta ya afya ni zaidi ya hili
Makala & UchambuziTangulizi

Matatizo sekta ya afya ni zaidi ya hili

Rais John Magufuli
Spread the love

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la magonjwa ya dharura katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora.

Akiwa katika eneo hilo 30 Januri 2021, Rais Magufuli, alinukuliwa akisema, madaktari waliokimbia hospitali hiyo na kujiunga na hospitali binafsi kwa kigezo cha kutafuta maslahi zaidi, watafutwe ili waweze kurejeshwa kazini.

Vinginevyo, Rais amesema, wizara ya afya isimamishe leseni ya udaktari ya madaktari hao na ikibidi, kuzifungia hospitali zote wanazochukua madaktari kutoka hospitali za umma.

Alisema, “wakati wa kusomesha hawatuchangii, tukishawasomesha wanakwenda kuwaiba, hii siyo sawa.”

Kwa maoni ya Rais Magufuli, kukimbia hospitali ya serikali na kujiunga na hospitali binafsi kwa kisingizio cha maslahi, ni kukosa uzalendo.

Sisi katika MwanaHALISI Online, tunatambua kuwa Serikali inatumia mamilioni ya shilingi, katika kuandaa watalaamu hawa.

Tunatambua kama alivyosema Rais, kuwa madaktari wote waliosoma nchini na hata baadhi ya waliosoma nje, walipata mkopo wa asilimia 100 wakati wakiwa masomoni.

Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya wa Tanzania

Hata hivyo, hatua yoyote ya kuwalazimisha madaktari kufanya kazi kwenye hospitali za serikali, haiwezi kumaliza tatizo lililopo. Yweza kuzalisha tatizo kubwa zaidi.

Hii ni kwa sababu, kinachokimbiza madaktari wengi hospitali za umma, hasa zile zilizoko wilayani na mikoani, ni pamoja na maslahi duni.

Kwamba, madaktari wengi, wanalalamikia mishahara midogo. Wanalalamikia ukosefu wa motisha, ikiwamo mafunzo na kutokuwapo kwa vifaa bora vya uchunguzi na tiba.

Hivyo basi, hatua ya serikali ya kuwalazimisha watalaamu hawa kufanyia kazi hospitali za umma, kunaweza kusababisha wengi wao wakaondoka nchini na kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Hilo likitokea, Serikali itashindwa kukusanya fedha ambazo madaktari hao wamekopeshwa.

Vilevile, kushindwa kwa madaktari hawa kulipa mikopo yao, kutasababisha Serikali kujipunguzia uwezo wake wa kusomesha madaktari wengine; na au wataalamu wa sekta mbalimbali.

Lakini kubwa zaidi, hatua hii ikitekelezwa, yaweza kuzalisha tatizo kubwa la uhaba wa madaktari nchini.

Pia, kinachoweza kufanywa na Serikali ni kujiuliza, kwa nini madaktari wanakwenda sekta binafsi? ikishapata majibu kama ni maslahi, mazingira bora ya kufanyia kazi, mafunzo kazini, inaweza kuyafanyia kazi ili kuwashawishi wasihame.

Kwa muktadha huo, kwa kuwa hospitali binafsi, nazo zinahudumia Watanzania, ni vema maelekezo haya yakaangaliwa kwa jicho jingine, ili kulinda wataalamu tulionao na kusaidia sekta binafsi kukua.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!