Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Maswali tata mauaji yaliyofanywa na askari Kigoma
Habari MchanganyikoTangulizi

Maswali tata mauaji yaliyofanywa na askari Kigoma

Spread the love

 

MAUAJI ya raia mmoja yaliyofanywa na askari wa jeshi la polisi nchini, pamoja na kujeruhiwa kwa raia wawili, katika uwanja wa michezo mkoani Kogoma, yamezidi kuibua utata. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Utata wa sasa unatokana na hatua ya polisi kudai kuwa askari wake walilazimika kutumia risasi, kuwatuliza washabiki wa timu mbili za mpira wa miguu, waliokuwa wameanza kuzomeana na kurushiana chupa za maji na mawe.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, tarehe 14 Machi 2022, muda wa saa 10 za jioni, katika uwanja wa Lake Tanganyika, kulitokea vurugu katika mechi ya fainali za kombe la kumuenzi Dk. Livingstone lililoandaliwa na Shirika la Joy The Havest, kati timu ya Mwandiga FC na Kipamba FC.

“Vurugu hizo zilisababishwa na kile kilichoelezwa na jeshi la polisi katika taarifa yake ya jana Jumanne tarehe 15 Machi 2022, kwamba kilichosababisha mauaji hayo, ni “mashabiki wa pande hizo mbili.”

Kauli ya jeshi hilo, kwamba ililazimika kuingilia kati vurugu hizo, lakini ghafla ziligeuka kuwa mauaji baada ya askari namba F.5123 D/CPL. Subira kufyatua risasi za moto, imechochea wito wa wananchi wa kutaka jeshi hilo, lifumuliwe na kuundwa upya.

 Kwamba, kile kinachoelezwa na polisi kuwa mauaji hayo yalitokana na askari huyo kupigwa kwa mawe kichwani na kuanguka chini, na hivyo kulazimika kutetea uhai wake na kujihami asinyang’anywe silaha yake na mashabiki, kimezidisha kuchochea moto wa suala hilo.

Aidha, mazingira ya tukio hilo sambamba na kile kinachoelezwa na polisi pamoja na mashuhuda, yanaibua maswali kadhaa yanayohitaji majibu.

Kwanza, mawe yanayodaiwa na polisi kuwa yalitumiwa na mashabiki hao kushambuliana, yalitoka wapi ndani ya uwanja wa soka?

Kwa tunavyofahamu viwanja vingi aina ya Lake Tanganyika, ni nadra sana kukuta mawe makubwa kiasi cha kuweza kurushwa na kumjeruhi mtu. Labda iwe kwamba mashabiki waliingia na mawe uwanjani na hili halijaelezwa kokote na taarifa ya polisi.

Wala jeshi hilo, halijatoa picha za video zinazowaonyesha washambiki wakirushia mawe, badala yake, picha zilizopo mitandaoni, zinawaonyesha washabiki wakishangaa hatua ya polisi kufyatua risasi.

Kama hiyo haitoshi, wakati polisi wanadai kulikuwa na urushianaji wa mawe uliotishia uhai wa washabiki na wanausalama waliokuwapo, picha zinawaonyesha baadhi ya wachezaji wakiendelea kuchezacheza mpira, jambo linathibitisha kuwa vurugu hizo hazikuwa kubwa kiasi cha kulazimisha polisi kutumia risasi za moto.

Pili, taarifa ya polisi inaeleza kuwa askari waliokuwepo uwanjani walizidiwa na kuita wenzao kuongeza nguvu. Lakini haisemi kama askari aliyefyatua risasi ni miongoni mwa waliokwenda kuongeza nguvu au waliozidiwa.

Hawasemi wakati askari mmoja anavamiwa, wenzake walikuwa wapi. Hawasemi kwanini mashabiki hawakuwavamia askari waliokuwepo tangu awali na waanze kumvamia huyu ambaye amekuja kuongeza nguvu? Hawaelezi walikokuwa wenzao hadi washindwe kumsaidia.

Tatu, jeshi hilo linasema, kabla ya ufyatuaji huo wa risasi za moto, jeshi hilo lilitumia mabomu ya machozi na sauti ya kuogofya, lakini halikufanikiwa kudhibiti vurugu hizo.

Hawaelezi mabomu ya machozi na sauti yalishindwaje kusambaratisha idadi ndogo ya watu waliokuwapo uwanjani, hadi wao kulazimika kutumia risasi za moto?

Kwa uhalisia wa uchache wa watu wanaoonekana kwenye video, hakuna mwenye akili timamu anayeweza kukubaliana na utetezi wa polisi kwenye mauaji yale. Kwamba, walishindwa kuwatuliza wananchi wale, pamoja na kutumia mabomu ya machozi? Haiwezekani.

Nne, jeshi la polisi limeeleza kuwa askari alifyatua risasi tisa hewani, lakini mashabiki hawakurudi nyuma bali waliendelea kumshambulia hadi alivyofyatua zingine tatu zilizosababisha madhara.

Haya ni tofauti na yanayoonekana kwenye video iliyotumwa na washabili waliokuwapo uwanjani, baada ya milio ya risasi kusikika.

Katika video hizo, watu wanaonekana wakianza kukimbia ovyo mara baada ya polisi kuanza kufyatua risasi. Na kwa uhalisia, ukisikia milio ya mabomu ya machozi na sauti ya kuogofya inatisha zaidi ya hata milio ya risasi.

Kwamba video inaonyesha watu wakitawanyika mara tu baada ya kuanza kusikika milio ya risasi na je, ilikuwaje wasitawanyike kwa mabomu ya machozi na sauti ya kuogofya au kwa risasi tisa za hewani?

Tano, suala lingine linaloacha maswali, ni kwanini mashabiki waache ugomvi wao na kuanza kumshambulia askari, wakati tunaambiwa vurugu zilikuwa baina ya mashabiki wa pande mbili? Na wa kwani mechi iliendelea hata baada ya tukio hilo?

Taarifa zinasema, mechi hiyo iliendelea licha ya kutokea kwa tukio hilo ambalo polisi wanadai kuwa askari wake alijeruhiwa vibaya na hadi jana bado alikuwa amelazwa hospitalini kwa matibabu.

Kwamba, iliwezekanaje jeshi la polisi kuacha mechi ile kuendelea licha ya kujua askari wake amejeruhiwa vibaya katika tukio hilo? Je, mechi iliendea bila mashabiki au waliendelea kuwepo?

Kama waliendelea kuwapo, tunarudi kule kule, kipi kilichosababisha vurugu? Kipi kilichowasukuma polisi kufyatua risasi?

Hakika, maswali haya hayawezi kujibiwa na jeshi la polisi lenyewe kwa kuwa wao ni sehemu ya watuhumiwa wa moja kwa moja wa tukio hilo.

Ndiyo maana wadau mbalimbali kikiwemo chama cha ACT- Wazalendo, kimependekeza kuundwa timu huru ya uchunguzi ili kuona nini chanzo na sababisho la mauaji hayo ya kizembe.

Kuundwa kwa tume kutasaidia siyo tu, kufahamika ukweli, bali kuwajibisha wote waliohusika, jambo ambalo litaweza kukomesha mauaji ya aina hiyo katika siku zijazo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!