December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maswali 6 tata kuapishwa Mdee na wenzake

Spread the love

HATUA ya wanachama 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nchini Tanzania, kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muuungano, kulikofanyika jana Jumanne jijini Dodoma, kumeibua maswali lukuki.  Anaripoti Regina Mkonde, Dar es  Salaam…(endelea).

Wabunge hao waliapishwa jana Jumanne, tarehe 24 Novemba 2020, viwanja vya Bunge jijini Dodoma na Spika Job Ndugai ambaye baada ya kumaliza kuwaapisha, aliahidi kuwapa “ushirikiano wote watakaouhitaji.”

Miongoni mwa waliopishwa kuwa wabunge, ni pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake taifa (Bawacha), Halima Mdee; Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Grace Tendega; Makamu Mwenyekiti wake, Hawa Subira Mwaifunga; Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Ester Bulaya na Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta  Lambat Kaiza.

Wengine walioapishwa, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Serengeti na Mjumbe wa Kamati Kuu, Esther  Matiko; Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wapo pia aliyekuwa mbunge wa Same Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka; Cecilia Pareso, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Lwamlaza, Stella Siyao, Felister  Njau na naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Kati ya wabunge hao 19 walioapishwa, 15 walikuwa wabunge waliokuwapo katika Bunge lililopita, huku wanne wakiwa wanaingia kwa mara ya kwanza.

Aidha, baadhi ya walioapishwa kuwa wabunge, ni wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema na watu ambao wako karibu na viongozi wa juu wa chama hicho, akiwamo mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, John John Mnyika.

Haya ndio baadhi ya maswali ambayo wananchi na wasomaji wa MwanaHALISI Online wanajiuliza. Yanaibuka na kuzua mjadala katika kipindi ambacho chama hicho, kimeitisha kikao maalum cha Kamati Kuu, Ijumaa ya tarehe 27 Novemba 2020, kujadili suala hilo.

Mkutano wa Kamati Kuu, umepangwa kutafanyika makao makuu ya chama hicho, Ufipa, jijini Dar es Salaam.  Watuhumiwa wote 19 wameitwa kujitetea:

Kwanza, nani mkweli kati ya wabunge hao wa Viti Maalumu, wanaodai wamefikia uamuzi huo wa kuapishwa kutokana na kupata baraka za chama chao na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe?

Hii ni kwa sababu, mara baada ya Mdee kuapishwa, alipewa nafasi na Spika wa Bunge kuzungumza kwa niaba ya wenzake. Akakishukuru Chadema na Mbowe kwa kuwaamini, na kuahidi kukiwakilisha vyema ndani ya Bunge.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Hata hivyo, anachokisema Mdee, kinatofautiana na kile alichokieleza Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, kwamba Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, hakijateua majina na kuyawasilisha Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC).

Je, kama Mdee anasema wabunge walioapishwa wanabaraka za chama hicho, huku Mnyika ambaye ni mtendaji mkuu wa Chadema, akieleza chama chake hakijapeleka majina, nani mkweli katika hili?

Pili, nani yuko nyuma ya mkakati huu ndani ya Chadema au nje ya chama hicho, ikiwa Kamati Kuu ya Chadema yenye mamlaka ya kuthibitisha majina ya wanachama wake wanaostahili kuteuliwa katika nafasi hizo na NEC, haikutihibitisha uteuzi wao?

Hapa utata unazidi kuongezeka hasa ikizingatiwa miongoni mwa wanachama hao 19, kuna wajumbe wa kamati kuu, ambao ni Mdee, Matiko, Bulaya na Tendega. Kama Kamati Kuu haikuteuwa, wamepata wapi ujasiri wa kwenda bungeni kuapishwa?

Mnyika anasema, kikao cha kamati kuu kilichofanyika mapema Novemba mwaka huu, hakikufikia maamuzi ya kupeleka majina. Bulaya alikuwapo. Mdee alikuwapo. Matiko alikuwapo na hata Tendega ambaye pia ni mjumbe wa sektarieti alikuwapo.

Kwa mujibu wa Mnyika, katika kikao hicho, kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Mbowe, maamuzi yalikuwa kupeleka majina ya wabunge wa viti maalum, kunakwenda sambasamba na kubariki matokeo ya uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba, ambao chama hicho kinadai kutoutambua.

Kwamba, kama haya ndio yaliyotokea, nani ndani ya Chadema walioshirikiana na Mdee, Tendega, Kunti na Agnesta, kupeleka majina NEC? Watachukuliwa hatua gani?

Tatu, orodha ya majina 19, iliwasilishwa na nani NEC?

Mnyika ambaye ndiye anapaswa kuwasilisha na kusaini fomu namba 8(d) ya kuteuliwa na chama, amekana kuzijaza fomu hizo za wanachama hao walioapishwa kuwa wabunge.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano tarehe 25 Novemba 2020 jijini Dar es Salaam, Mnyika amesema, NEC iliwasilisha ofisini kwake fomu hizo 113 ambazo zilipaswa kujazwa na wateuliwa kisha yeye kuzisaini.

Anaongeza, “lakini fomu hizi zote, bado ninazo. NEC itueleze ni nani amesaini hizo fomu na zimetoka wapi ikiwa walizonipa bado zipo?”

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera

Nne, miongoni mwa wabunge walioapishwa ni Nusrat Hanje, ambaye alikuwa gerezani tangu Julai 2020. Alichiwa huru siku moja kabla ya kuapishwa.

Nusrati aliachiwa huru yeye na wenzake usiku wa tarehe 23 Novemba 2020, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwafutia mashtaka, kisha kupishwa mchana wa tarehe 24 Novemba 2020.

Nusrat hakushiriki mchakato wa ndani ya chama wa kuwapata wagombea viti maalum, kwani wakati mchakato ukiendelea yeye alikuwa mahabusu mkoani Singida.

Lakini Hanje alitolewa gerezani tarehe 23 usiku ili kesho yake apelekwe kuapa. Spika wa Bunge, Job Ndugai anasema, amepokea majina na fomu za wabunge kutoka NEC tarehe 20 Novemba.

Kama Nusrat ametolewa gerezani tarehe 23, fomu yake alijaza lini? Hii fomu Na. 8(d) ambayo walioteuliwa kwa viti maalumu huwa wanajaza. Sasa unajiuliza, Nusrat alijazaje ya kwake akiwa gerezani?

Sehemu C ya fomu hiyo, inataka uthibitisho wa vyama ambapo katibu mkuu au naibu wake husaini na kugonga mhuri. Kama Nusrat alitoka gerezani usiku na kesho yake akaapishwa, fomu yake ilithibitishwa na nani ndani ya Chadema?

Aidha, fomu hiyo inataka uthibitisho wa kiapo mbele ya Hakimu. Fomu ya Nusrat na wengine, zimepata muhuri wa mahakama? Zimepata mhuli wa Chadema?

Katika hili, Mnyika anajaribu kueleza, kwamba “ni dhahiri Nusrat alijaziwa fomu yake akiwa gerezani. Na waliomsaidia kujaza wakamsaidia kughushi saini na mihuri ya katibu mkuu, wakamsaidia kughushi saini na mihuri ya Mahakama maana hakuna Hakimu anayeweza kusaini usiku wa manane.”

Anasema, “hapa kuna jinai kubwa ya kughushi inayohusisha hadi mhimili muhimu kama mahakama na NEC.”

Tano, Ibara ya 78 (1)(3) na (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia utaratibu wa uchaguzi wa wabunge wa Viti Maalum, kwamba chama kitawasilisha majina NEC ambayo kabla ya kufanya uteuzi, itashauriana na chama husika.

Je, NEC kabla ya kufanya uteuzi huo, ilishauriana na Chadema? Kama ndio ilishauriana na nani? Ilitumia njia gani? Kama haikufanya hivyo, haioni hapo kuwa imekiuka masharti haya ya Katiba?

Katika mkutano wake na waandishi, Mnyika amesema, NEC iliwaandikia barua tarehe 10 Novemba 2020, kuwajulisha kutopokea majina ya Viti Maalum na kuwasisitiza kufanya hivyo.

Kama NEC ilifanya hivyo na ili kuwepo kwa mizania ya uwazi, kwa nini haikuweka wazi mchakato huu ili kutimiza kile kinachoelezwa kuwa uchaguzi uwe huru, amani na haki?

Sita, nini hatma ya wanasiasa hao 19 endapo, Kamati Kuu, itaamua kuwafukuzwa?

Je, wataendelea kuwa wabunge kama ilivyotokea huko nyuma kwa baadhi ya wanachama wa Chadema waliofukuzwa?
Miongoni mwa waliofukuzwa katika Bunge la 11 uanachama wa Chadema na kisha wakaendelea na ubunge, ni Anthony Komu (Moshi Vijijini), (Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini), Joseph Seasini (Rombo) na David Silinde (Momba).

Wanasiasa hao walifukuzwa uanachama baada ya kukaidi maagizo ya Chadema kutoshiriki vikao vya Bunge kwa ajili ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corova (Covid-19).

error: Content is protected !!