May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

MASUJIRO HASHIMOTO: Baba wa NISSAN aliyelelewa na Japan

Spread the love

Breviare ni kitabu maalum cha Kikristo kwa ajili ya sala za asubuhi, mchana na jioni pamoja na nyongeza ya vipindi vingine kwa nyakati maalumu kama vile Kwaresma, Pasaka, Majilio na vingine.

Ni maarufu kama ‘kitabu cha masigu. Ndani yake kuna kiitikio kimoja kinasema “kama mtu akikualika kwenye harusi, keti katika kiti cha mwisho ili akikuona akuite akisema; ‘rafiki njoo hapa mbele mahali pa heshima zaidi.”

Ndivyo alivyofanya kijana Masujiro mwana wa Mzee Hashimoto, nchini Japan.

Japan imejitahidi kuthamini wabunifu wake hasa upande wa fundi stadi. Leo tunaona kampuni ya Toyota ikifanya vizuri sokoni, vilevile kampuni ya Yamaha nayo haiko nyuma.

Kadhalika kampuni ya Nissan, Suzuki, Sony, Panasonic na nyingine nyingi. Japan ilidhamiria kuimarisha maendeleo ya viwanda.

Shule nyingi za ufundi stadi zilifunguliwa. Mmoja kati ya walinufaika ni kijana Masujiro Hashimoto. Yeye alizaliwa mwaka 1875 mjini Okazaki, Japan.

Masujiro Hashimoto alikua vema na kupata elimu iliyomsaidia sana. Licha ya kuwa mwanajeshi lakini aliona vema aanzishe kampuni yake.

Wizara ya Kilimo na Biashara ilimsomesha kijana huyo huko New York, Marekani, kwa kisomo cha miaka mitatu. Tena ilimpangia kozi ya kusoma ambayo ni Umakanika ili akirejea nyumbani awape wenzake ujunzi ili nchi ipate wataalamu wengi zaidi.

Aliitumia vema nafasi ile na kusoma kilichotakiwa. Baada ya kuhitimu alirudi nyumbani kwao Japan na kufanya kazi mbalimbali kama vile uundaji wa mashine, bunduki kwa ajili jeshi, na nyinginezo. Nchi ikafurahi na ikaona kuwa imlea Masujiro na akaleleka vizuri.

Baada ya kufanya kazi Serikalini kwa muda mrefu hatimaye Masujiro akaanza safari ya ujasiriamali.

Akajikita katika Umakanika. Kampuni iliitwa KWAISHINSHA MOTOR WORKS. Hapo kazi ikaanza.

Masujiro Hashimoto akaamua kuwaita rafiki zake wa utotoni aliocheza nao daima ili wawe sehemu ya kampuni hiyo.

Yeye kama kiongozi akawapa majukumu kwa wenzake kila mmoja na kitengo chake. Rafiki zake hao ni Kenjiro Den, Rokuro Aoyama na Meitano Takeuchi.

Kwa pamoja vijana hao walichapa kazi kwa bidii. Baadae walibadilisha jina la kampuni kuwa NISSAN MOTOR WORKS COMPANY. Ndiyo hii NISSAN inayoonekana leo na magari yake mengi duniani kote.

Urafiki wa utotoni kumbe una manufaa hivi mkiaminiana. Kubwa ni wote kuwa tayari kutoa na kupokea ujuzi. Kuwa pamoja na kufanya kazi kama timu.Makala haya yameandaliwa na Kizito Mpangala ‘Jalimu’

error: Content is protected !!