August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mastaa wa muziki Afrika waachia African Lullabies Part 2 kwa kishindo

Spread the love

KIKOSI kazi cha kusherehekea mwezi wa Afrika kwenye mkusanyiko wa nyimbo zenye mahadhi ya Kiafrika zilizopewa jina la African Lullabies Part 2, kimeachia toleo la pili kutoka kwa kizazi cha muziki wa Kiafrika. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Mastaa kadhaa kutoka pande mbalimbali za Afrika wameshiriki katika ujio huo, wakiwemo Asa, Ayra Starr, Karun, Teni, Simi, WurlD, Olayinka Ehi, Tresor, Manana, Aymos na Ntsika.

 

Wakati katika sehemu ya kwanza – African Lullabies Part 1 iliangazia utunzi asilia wa waimbaji na watunzi wa nyimbo wa Afrika Kusini huku ikiimbwa katika lugha mbalimbali, safari hii inapanuka zaidi ya mipaka ya Afrika Kusini na kutoa toleo tofauti la muziki wa watoto katika lugha mbalimbali za Kiafrika.

Nyimbo zote ni tungo asili za wasanii, zikichorwa kutokana na uzoefu wao katika ngano za Kiafrika, huku zingine zikiwa ni tafsiri za nyenzo zilizotolewa hapo awali zilizopangwa na kurekodiwa tena.

Ikiwa ni mara ya kwanza kwa msanii Karun kutunga wimbo wa kwanza kwa ajili ya watoto, alisema: “Ilinifurahisha sana pale nilipotakiwa kutengeneza wimbo kwa ajili ya watoto, Huu ni wimbo wangu wa kwanza wa watoto, sikuwahi kufikiria ningefanya.

“Nimefurahia sana kufanya muziki huu wa utulivu. Sijawahi kuona muziki wa watoto kama kitu ambacho ningefanya lakini nilipopewa nafasi nimeonyesha uwezo wangu wote. Binafsi nina mtoto wa kiume na ninapenda sana watoto, imekuwa kitu kizuri sana kwangu.”

Karun ameongeza kusema, amejifunza mengi kutoka kwake mwenyewe wakati alipokuwa akiandika wimbo huo.

“Nimetayarisha wimbo wote mwenyewe, napenda sana mikito mizuri, kwahiyo nilichofanya ni kucheza na mikito ya aina mbalimbali wakati wa utayarishaji. Kuna mengi ya kujifunza katika kibao hiki. Pia nilijifunza kuna mengi zaidi ninayohitaji kuunganisha katika lugha yangu ya mama ya Kikikuyu.

“Kuna wakati ilibidi bibi yangu kunikumbusha baadhi ya maneno. Kikuyu ni lugha yangu ya kwanza lakini niliisahau muda mrefu uliopita, hivyo nilijifunza kuwa bado ninaunganishwa nayo.”

Kwa upande wa msanii Ayra Starr amesema, “Shangazi yangu ni kila kitu kwangu na alijifungua miezi mitatu iliyopita. Kwahiyo ikawa ni kama nimemtengenezea mpwa wangu wimbo. Nakumbuka wakati tunakua, tulitunga nyimbo sisi wenyewe, shuleni pia tulikuwa tukitengeneza nyimbo zetu wenyewe kwa sababu hatukutaka kuimba “Twinkle, twinkle, little star.”

Majina ya wasanii walioshiriki kwenye albamu hiyo na nyimbo zao kwenye mabano ni pamoja na Psalms of Suli (Hello Little One), Teni (One Day), Simi (Iya Ni Wura), Karun (Dream Lullaby (Wakarirü) na Tresor (La Vie Est Belle).

Wengine ni Olayinka Ehi (Sweet One), Asa (Little Darling), Ayra Starr (Stars), Aymos (Lullaby Song), Ntsika (Busuku Benzolo), WurlD (Never Alone) na Manana (In The Morning). Kusikiliza ingia hapa: https://platoon.lnk.to/African-Lullabies-Part2.

error: Content is protected !!