September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Masikini Dk. Shein

Spread the love

MZIMU wa kukataliwa umeendelea kumwandama Dk. Ali Mohammed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kutokana na kushikilia mamlaka ya urais wa visiwa hivyo kwa hila, anaandika Faki Sosi.

Wakati Chama cha Wananchi (CUF) kikipuuza urais wa Dk. Shein baada ya kutunukiwa nafasi hiyo na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mataifa ya nje na wahisani wakionesha msimamo wa kugomea kupondwa kwa demokrasia visiwani humo, Chama cha Demokarsia na Maendeleo (Chadema) kimemkataa rasmi.

Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema ametoa msimamo huo jana mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma akiwa na manaibu wake John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Chadema kimesema kuwa, hakitampa ushirikiano wowote Dk. Shein kwenye serikali aliyoiunda na kwamba, msimamo wa Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa mgombea urais visiwani humo kupitia CUF ndio msimao wa chama hicho.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF aligoma kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu baada ya ZEC kufuta matokeo halali ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana ambao unatajwa kumpa ushindi mgombea wa CUF.

Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alifuta matokeo hayo akiwa tayari ametangaza kwa zaidi ya nusu ya majimbo visiwani humo.

Jecha mwaka 2010 aliwahi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta nafasi ya kuteuliwa kugombea ubunge kwenye Jimbo la Amani, Unguja lakini wana-CCM wa jimbo hilo walimtosa.

Kwenye uchaguzi wa 20 Machi mwaka huu Jecha alimtangaza Dk. Shein (CCM) kuwa mshindi na kudai alipata kura 299,982 sawa na asilimia 91.

Alimtangaza Hamad Rashid Mohamed (ADC) ambaye alifukuzwa na CUF kutokana na tuhuma za usaliti katika chama hicho kushika nafasi ya pili kwa kura 9,734 sawa na asilimia 3.0.

Pia Jecha alimtangaza Maalim Seif kwamba alipata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9 ambapo alidai, wapiga kura walikuwa 503,580 na kwamba, jumla ya kura zilikuwa 341,885 sawa na asilimia 7.9 huku kura zilizoharibika ni 13,538 sawa na asilimia 4.0 na kura halali zilikuwa 328,327 sawa na asilimia 96.0.

Mwalimu amesema, hali ya Zanzibar ni tofauti na ambavyo viongozi wa CCM wanavyonadi kwenye vyombo vya habari na kwamba, anatarajia hali kuwa mbaya zaidi baada ya tamko hiyo na kuwa, tayari Wazanzibari wameanza kumatenga Dk. Sheini.

Naibu huyo wa Zanzibar amezema kuwa, Dk. Shein na CCM yake wamewarejesha Wazanzibari katika masiha ya mwaka 1995 ya uhasama na kabla ya kuunda kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo.

Hatua ya Dk. Shein kupuuza uchaguzi wa kidemokarsia na kung’ang’ania madaraka visiwani humo tayari imeitia hasara nchi ambapo wahisani wamegoma kulisaidia taifa.

Bodi ya Taasisi ya Changamoto ya Milenia (Millennium Challenge Corporation) ya Marekani iliamua kusitisha misaada yake kutokana kuvurugwa kwa demokrasia hususani uamuzi wa serikali kurudia uchaguzi wa Zanzibar Machi 20 mwaka huu pia uamuzi wa serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya mwaka 2015, sheria ambayo inakandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu. Nchi nane kati ya 16 zimeeleza waziwazi kutoishaidia Tanzania.

Hata hivyo, jana asubuhi Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo akiwa Dodoma ameeleza kuwa, Serikali ya Jamhari ya Muungano wa Tanzania inatikisika kutokana na kukosa misaada lakini pia mapato yake ya kodi kuendelea kushuka kila mwezi.

“…kwa mfano wakati Rais Magufuli anaingia madarakani alitegeme mapato ya ndani yatakuwa Sh. 1.6 trilioni kwa mwezi, kwa kiwango hicho serikali ingeweza kukusanya Sh. 19 trilioni kwa mwaka.

“Lakini Februali yalishuka mpaka kuwa trilioni 1.4, Machi trilioni 1.2 trilioni na mwezi Aprili yalishuka tena na kuwa trilioni 1.1. Taarifa zilizopo kutoka mashirika ya fedha na mashirika mengine ya hiyari zinaeleza kwamba, mapato ya serikali hayawezi kuzidi Sh. 12 trilioni kwa mwaka,” amesema Kubenea.

error: Content is protected !!