August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mashtaka mapya 7 ya Sabaya na wezake, mvutano waibuka

Spread the love

 

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wakikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo kuunda genge la uharifu, kupokea rushwa ya Sh.30 milioni na utakatishaji fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea)

Sabaya amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano tarehe 01 Juni 2022 saa 5:35 asubuhi akiwa kwenye gari la polisi na kupelekwa moja kwa moja chumba cha mahakama akiwa chini ya ulinzi mkali.

Wamesomewa mashtaka na wenzake Silivester Nyegu, John Aweeyo, Nathan Msuya na Antero Assey kuanzia saa 5:55 hadi saa 6:45 mchana na mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka. Hata hivyo, Antero Assey hakuwepo mahakamani.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, shitaka la kwanza ni la kuunda genge la uharifu linalowahusu washitakiwa wote ambapo Februari 2021, Sabaya akiwa mtumishi wa umma kama mkuu wa wilaya ya Hai alikiuka majukumu yake ya kiutendaji kwa makusudi na kwa nia ya kutekeleza jinai walijipatia Sh.30 milioni.

Shitaka la pili linamhusu Sabaya peke yake akidaiwa Februari 2021 wilayani Hai kwa nia ya kutenda kosa alishawishi na kudai rushwa ya Sh.30 milioni kutoka kwa Godbless Swain tarehe hiyo hiyo alijipatisa Sh.30 milioni kama rushwa kutoka kwa Elibariki Swai kwa nia ya kuzuia taaarifa za kiuchunguzi kuhusiana na ukwepaji wa kodi.

Shitaka la tatu na la nne liliwahusu washitakiwa wanne, Silvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey ambao wanadiawa kwa pamoja kuwa Februari 2021 wilayani Hai walisaidia kutendeka kwa jinai.

Wanadaiwa katika tarehe hiyo washitakiwa hao walimsaidia Sabaya kuweza kushawishi na kumsaidia kupata Sh.30 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Alex Swai huku pia wakidaiwa kumsaidia Sabaya kujipatia manufaa asiyostahili kwa kujipatia Sh.30 milioni kutoka kwa Alex Swai.

Sabaya pia anadaiwa katika shitaka la sita linalomhusu yeye mwenyewe alitenda kinyume na na mamlaka yake kwa kutumia nafasi yake kama mkuu wa wilaya kwamba alinajisi nafasi yake ya mkuu wa wilaya kwa kuanzisha mashitaka dhidi ya Alex Swai kuwa amekwepa kodi na kujipatia Sh.30 milioni kwa manufaa yake na wenzake wanne.

Shitaka la saba ni la utakatishaji fedha lanalowahusu washitakiwa wote ambako Februari 2021 wilayani Hai kwa pamoja na kwa nia moja walijipatia Sh.30 milioni huku wakijua fedha hizo ni zao la uharifu.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya uhujumu uchumi hadi kupata kibali cha Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mara baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka yao, Hellen Mahuna, wakili anayewatetea washitakiwa hao alidai kuwepo na ukiukwaji wa taratibu za wateja wake kukamatwa na kufikishwa mahakamani mjini Moshi.

Lengai ole Sabaya

Amedai mahakama ya hakimu mkazi Arusha haikutoa kibali cha wateja wake kuchukuliwa kutoka Gereza Kuu la Kisongo mkoani Arusha na kupelekwa Gereza Kuu la Karanga mkoani Kilimanjaro.

Pia akadai, mawakili wa washitakiwa hawakupewa taarifa juu ya wateja wao kuchukuliwa kutoka Arusha na kwenda kusomewa mashitaka mkoani Kilimanjaro hoja ambazo upande wa mashitaka ulidai hazina mashiko na hazina miguu ya kusimama kisheria.

Akijibu hoja hizo, Kweka amesema hoja kwamba mawakili wa upande wa utetezi hawajapewa taarifa si za kweli kwani Hellen ndiyo wakili wao na hata washitakiwa hawajakana kuwa hellen ni wakili wao.

Kuhusu kesi inayowakabili washitakiwa huko Arusha, Kweka amesema hizo ni kesi mbili tofauti na zinaendeshwa kwenye mahakama mbili tofauti na kwamba mahakama za hakimu mkazi zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria na zinayo maeelekezo ya namna ya kuendesha mashauri.

Amesema shitaka wanaloshitakiwa nalo washitakiwa haliko kwenye mamlaka ya hakimu mkazi Arusha na mamlaka ya hakimu kazi wa Arusha yanaishia eneo la KIA ambako ndiyo ulipo mpaka wa mkoa wa Arusha na Kilimanjaro.

Lengai Ole Sabaya akiwa mahakamani Arusha

Akitoa uamuzi juu ya hoja zilizotolewa na upande wautetezi, Hakimu Mshasha alikubaliana na hoja za upande wa mashitaka kuwa mahakama ya hakimu mkazi Moshi haikuhitaji kupata kibali kutoka mahakama ya hakimu mkazi Arusha.

Amesema mahakama inayo mamlaka ya kuwaita washitakiwa na ilimwandikia barua mkuu wa gereza la Kisongo kuwaomba washitakiwa hao na kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachoilazimisha mahakama ya hakimu mkazi Moshi kuomba kibali kutoka kwa mahakama ya hakimu mkazi Arusha.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumanne ya tarehe 7 Juni 2022 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote wakapelekwa Gereza Kuu la Karanga ambako sassa wataanza maisha mapya kwenye gereza hilo baada ya kukaa muda mrefu gereza la Kisongo Arusha.

Aidha, Sabaya anakabiliwa na kesi nyingine Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya uhujumu uchumi ampo hukumu ya kesi hiyo imepangwa kutolewa tarehe 10 Juni 2022 baada ya kuahirishwa jana Jumanne.

Hukumu hiyo ni kesi ya pili ikitanguliwa na ile ya awalimu mahakamani hapo aliyohukumiwa miaka 30 gerezani lakini alishinda rufaa Mahakama Kuu kwenye kesi hiyo.

error: Content is protected !!