MAHAKAMA ya Rufaa nchini Tanzania, imetupilia mbali rufaa ya Serikali dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kufuta mashtaka 14 katika Kesi ya Jinai Na. 121/2021, inayowakabili Masheikh 23 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 19 Mei 2021 na Mwanasheria Kiongozi wa Jopo la Mawakili tisa wanaowatetea Masheikh hao, Juma Nasoro, wakati akizungumza na MwanaHALISI Online.
“Tumeshinda rufaa, masheikh wameshinda, uamuzi ulisema kwamba upande wa Jamhuri hawana haki kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu kufuta mashtaka 14, kwa sababu uamuzi ule haukumaliza kesi,” amesema Nasoro.
Nasoro amesema, kwa sasa masheikh hao wanabaki na mashtaka 11 ya makosa ya ugaidi, katika kesi inayowakabili Mahakama Kuu, wanayodaiwa kutenda katika nyakati tofauti Tanzania Bara.
Wakili huyo amesema, mashtaka 14 yaliyofutwa na Mahakama Kuu, ni yale ambayo makosa yake yanadaiwa kutendwa Zanzibar.
“Baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa tuanarudi Mahakama Kuu kuendelea na mashtaka ya mwanzo 11, ya makosa yote ya ugaidi yanayodaiwa kufanyika Bara, mashtaka 14 yaliyoondolewa ni yale ya makosa ya ugaidi yanayodaiwa kufanyika Zanzibar,” amesema Nasoro.
Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwafutia mashtaka 14 masheikh hao, ulitolewa na Jaji Mustapha Ismail, tarehe 23 Aprili 2021.
Masheikh hao wa uamsho walioko mahabusu tangu 2012, wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, walijihusisha na makosa ya ugaidi, kinyume na kifungu cha 27 (c), cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Leave a comment