MASHIRIKA ya Umma yatalazimishwa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) kwa kuwa sheria inawataka hivyo na ndiyo maana hata wabunge wamejiunga huko, anaandika Dany Tibason.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye amesema ni lazima kwa mashirika ya umma kujiunga na NHIF.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ulanga, Gudluck Mlinga ambaye alihoji ni kitu gani kinashindikana kwa mashirika hayo kujiunga na NHIF.
“Ninawathibitishia kwamba mashirika ya umma kujiunga na NHIF si hiari na hivi sasa nimetoka kufanya mazungumzo na na Waziri wa Fedha. Lazima tutumie bidhaa na huduma zinazozalishwa na serikali,” amesema Ummy.
Katika swali la msingi, Mlinga alihoji hadi sasa ni taasisi na mashirika ya umma mangapi yamejiunga na mfuko huo na mashirika mangapi hayajajiunga na mfuko huo na juhudi gani zinachukuliwa kuwalazimisha wajiunge.
Katika jibu la msingi, Naibu Waziri katika wizara hiyo, Dk. Hamisi Kigwangalla alikiri mfuko huo NHIF ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia matibabu kwa watumishi wa serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini.
Dk. Kigwangala amesema hadi kufikia Machi mwaka huu idadi ya wanachama katika mfuko ni 792,987 kutoka wanachama 474,760 mwaka 2012.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, mfuko umefanya maboresho mbalimbali ya vitita vya mafao na namna ya kuchangia kwa makundi mbalimbali ya jamii.
“Maboresho haya yamewezesha kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanachama walio katika mfumo huu wa bima ya afya nchini na kufanya manufaika kufikia asilimia nane,” amesema.
Naibu Waziri aliyataja mashirika, taasisi na idara za serikali ambayo hayajajiunga na mfuko huo yapo 23 yakiwemo TRA, BoT, Tanesco, NHC, TPA, PSPF, LAPF,PPF, EWURA, NCA na GEPF.
Leave a comment