October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mashine ya kisasa kupima UVIKO-19 yazinduliwa Zanzibar

Spread the love

SERIKALI ya Zanzibar, imezindua rasmi matumizi ya teknolojia mpya inayotambua maambukizi ya virusi vya korona (UVIKO-19) kupitia vipimo vya smaku umeme yaani electromagnetic. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Tofauti na zile nyingine, teknolojia hii, haihitaji msafiri kuchukuliwa sampuli ya vipimo kupitia mdomoni na au puani, na bila mhusika kuguswa.

Msafiri anaweza kupimwa akiwa umbali wa mita moja na majibu yake yakapatikana papo kwa papo.

Hii ni mara ya kwanza kwa teknolojia hii kutumika barani Afrika na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ndio unaandika historia ya kuwa uwanja wa kwanza wa kimataifa nchini Tanzania kuwa na teknolojia hiyo, ambayo imekuja kwa msaada kutoka serikali ya Abu Dhabi.

Mkurugenzi wa mradi huo, Dad Karim Mulla anasema, utafiti uliosababisha kupatikana kwa teknolojia hii umefanyika nchini Abu Dhabi na umegharimu takriban dola za kimarekani bilioni moja.

Inaaminika, matumizi ya teknolojia hiyo, yanaweza kuleta afueni kubwa kwa wasafiri ambao kwa sasa wataweza kuendelea na safari zao kwa haraka zaidi bila usumbufu na kupoteza muda.

Zanzibar na Abu Dhabi wamekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria ambapo ni jambo la kawaida kila mwaka kwa kisiwa hicho kupokea maelfu ya wageni kutoka nchi hizo mbili.

Kundi la kwanza la wageni lililotumia teknolojia hiyo, limetua mjini Uguja kupitia shirika la ndege la Fly Dubai mapema leo asubuhi ya Jumatano, tarehe 16 Februari 2022.

“Ni teknolojia nzuri. Inatoa majibu haraka sana, kwa kweli hata sikujua kama wanapima, nilihisi wananipiga picha tu. Nimefurahi,” anasema mmoja wa wasafiri kutoka Saudi Arabia.

Wakati huo huo, waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassoro Mazrui amesema mpaka sasa, Zanzibar haina mgonjwa mwenye maambukizi ya UVIKO-19 tangu Januari 2022, hivyo ni muhimu kwa serikali kukumbatia teknolojia ambayo itawaweka salama wazanzibar na wageni.

Zanzibar, kama maeneo mengine ya Tanzania, ilikumbwa na wingi la maambukizi ya UVIKO-19 tangu kuanza kuibuka kwa kirusi hicho.

Mwaka jana, wakati kama huu, Zanzibar ilimpoteza makamu wake wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia tarehe 17 Februari, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, wakati akipatiwa matibabu ya maambukizi ya UVIKO-19.

error: Content is protected !!