July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Masheikh: Wananchi wasishinikizwe kura ya maoni

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislam, Sheikh Khamisi Mataka

Spread the love

TAASISI ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislam nchini, imewataka viongozi wa dini, kuwahamasisha waumini wao kuisoma Katiba iliyopendekezwa bila kuwapa shinikizo. Anaandika Mwandishi wetu … (endelea).

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Khamisi Mataka wakati akijibu tamko la Jukwaa la Kikristo Tanzania kuhusu Mahakama ya Kadhi na Katiba mpya inayopendekezwa.

Sheikh Mataka amesema viongozi wa dini wana wajibu kuhakikisha Watanzania wanapata elimu ya katiba iliyopendekezwa ili wawe na uwezo na uhuru wa kuchagua kile wanachokiona kina manufaa kwao bila kuwepo shinikizo la kiimani.

“Binadamu wote wana uwezo wa kufikiri, hivyo haina sababu kuleta mashinikizo ya kiimani. Si mimi hata Mwadhama Polcarp Kardinali Pengo naye alisistiza tusiwagawe waumini bali tuwaelekeze,” amesema.

Kauli ya Sheikh Mataka imekuja siku chache tangu Jukwaa hilo kutoa tamko kupinga kuwepo kwa mahakama ya kadhi nchini kwa kile walichodai ni uvunjifu wa Katiba.

Taasisi hiyo ya masheikh imepinga tamko hilo kwa kile walichodai kwamba Sheria za Kiislamu ni moja ya vyanzo vya Sheria za Tanzania kama ilivyo kwa “Common Law “ za England.

“Ndio maana Mahakama za Tanzania zimekuwa zikizitumia sheria hizo tangu kuhukumu kesi za Waislamu kuhusu ndoa, talaka na mirathi toka 1963 baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Mahakama za Mahakimu ya 1963 na kufuatiwa na Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu ya 1964 na kuhitimishwa na sheria ya ndoa.

“Tatizo liliopo, kesi hizo zinahukumiwa na hakimu wasio na elimu, ujuzi wala sifa za kuwa makadhi kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu, na huo ndio msingi wa Waislamu kudai uwepo wa Mahakama ya Kadhi ili tuwe na wataalumu,” amesema Sheikh Mataka.

Ameongeza kuwa baada ya kulisoma na kutafakari tamko la maskofu walibaini kwamba maaskofu walijisahau kuwa wao ni viongozi wa dini na kiroho ambao wanatakiwa wawe tayari kumpokea yeyote na kumpa neno la hekima lenye faraja bila kujali itikadi au chama chake cha siasa badala yake walizingatia utashi wa kisiasa.

Ameongeza kuwa maaskofu walitumia msukumo wa kiimani na nyumba za ibada ili kuwazuia waislamu wasipate haki ya kuwa na Mahakama ya Kadhi na kutoa madai kuwa walipewa rushwa ili kufanikisha mchakato wa Katiba iliyopendekezwa, kauli ambayo amedai kuwa iliwakera.

“Tumesikitishwa na tamko lao, linaloonyesha kuwadhalilisha waislamu, madai yao yanaonyesha dharau, kiburi na kutowaheshimu waislamu, jambo ambalo lina athari mbaya kwa mahusiano yetu yaliyodumu muda mrefu baina ya Waislamu na Wakristu,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Sheikh Mataka, suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu wala halihitaji ridhaa ya wasiokuwa waislamu kwa kile alichodai wao hawajawahi kuombwa ridhaa yao katika yale ambayo serikali imewafanyia na makanisa yao.

error: Content is protected !!