Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Masheikh Uamsho wamwangukia Samia, waeleza walivyotoswa na JK, JPM
Habari MchanganyikoTangulizi

Masheikh Uamsho wamwangukia Samia, waeleza walivyotoswa na JK, JPM

Spread the love

 

MASHEIKH 18 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), wameeleza namna Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, walivyokataa kusikiliza maombi yao, kuhusu mashtaka ya ugaidi, yaliyokuwa yanawakabili tangu 2012. Anaripoti Mwandishi, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi, tarehe 17 Juni 2021, kwa niaba ya Masheikh hao, Farid Hadi, amesema 2012 wakati Kikwete akiwa madarakani, walimuomba aunde tume ya kuchunguza tuhuma zao, lakini hakuwasikiliza.

Sheikh Farid amesema ombi hilo walilitoa kwa mara ya kwanza, walivyopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe visiwani Zanzibar, Oktoba 2012, wakati Kikwete akiwa Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania.

“Wakati wa Kikwete mimi nililpopanda mahakamani mara ya kwanza kabisa, nilimuomba afanye jitihada aunde tume achunguze hili suala, hakuna aliyeitika,” amesema Sheikh Farid.

Baada ya ombi hilo kukataliwa na Kikwete, Sheih Farid amesema alipoingia madarakani Magufuli, walimuandikia barua kumuomba afuatilie suala lao, lakini hakuwajibu.

“Amekuja mheshimiwa Magufuli, mimi binafsi nimemuandikia mpaka barua ya kumuomba alitizame hili, lakini hakuna majibu yoyote,” amesema Sheikh Farid.

Magufuli alifariki dunia akiwa madarakani tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mwili wa Magufuli aliyefariki baada ya kuiongoza Tanzania, muda wa miaka mitano na miezi mitano mfululizo (Novemba 2015-Machi 2021), ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

Sheikh Farid amesema baada ya Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani kufuatia kifo cha Magufuli, mwenendo wa mashtaka yao ulianza kwenda vizuri, hadi tarehe 15 Juni 2021, yalivyofutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu

“Samia ameingia madarakani kuanzia tarehe 19 Machi 2021, siku aliyoapa. Sisi tarehe 12 Aprili 2021, ilianza kusikilizwa kesi yetu, ikaanza kusikilziwa rasmi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ijapokuwa ilianza anza kwa nyakati za mbali. Ni kama ilisukumwa na baada ya hapo ikalala,” amesema Sheikh Farid.

Sheikh Farid amesema“Rais Samia ni kiongozi imara, Amiri Jeshi Mkuu mtiifu kabisa, sababu zamani utawala ulikuwepo lakini hatukusikilizwa.”
Sheikh Farid ameiomba Serikali ya Rais Samia, iwafikirie kwa kuwapa kifuta machozi, kufuatia athari walizopata wakiwa mahabusu gerezani kwa muda mrefu.

“Lakini tunasema busara lazima iwepo, sababu tumeathirika, tumepoteza mamilioni ya pesa na mali tulizokuwa tunamiliki. Biashara zimekufa kabisa, tunaanza sifuri. Mimi nilikuwa namiliki gari za tax tano zimekufilia mbali,” amesema Sheikh Farid na kuongeza:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

“Daladala tatu zimekufilia mbali, biashara zote zimekufa nakuja naanza upya. Lazima Serikali imeliona hilo bila shaka imetafakari hilo. Naaamini busara ndiyo inajenga amani, mapenzi nauvumilivu.”

DPP Mwakitalu aliwafutia viongozi hao 18 mashtaka, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kuwafutia mashtaka 14 kati ya 25 yaliyokuwa yanawakabili, kwenye Kesi ya Jinai 121/2021, tarehe 23 Aprili 2021.

Mahakama hiyo ilifuta mashtaka hayo, kwa maelezo kwamba hayakufanyika Tanzania Bara, hivyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa yaliyofanywa visiwani Zanzibar.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

DPP Mwakitalu alisema, mashtaka 11 yaliyosalia hayakuwa na nguvu, sababu iliyopelekea ofisi yake kuyafuta.

Masheikh hao wameachwa huru baada ya kusota mahabusu kwa miaka minane, tangu walipokamatwa katika nyakati tofauti kati ya 2012 na 2014.

Katika kesi hiyo, walikuwa wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, walijihusisha na makosa ya ugaidi, kinyume na kifungu cha 27 (c), cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

1 Comment

  • Mahabusu miaka minane??? Jamani nyinyi watetezi wa haki za binadamu kitaifa na kimataifa hamuoni aibu? Mmekaa kimya? Marekani iko bizy kuzisakama China na Urusi tu. Huku hamuoni?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari Mchanganyiko

DC ampongeza Dk. Rose Rwakatare kwa kusaidia waathirika wa mafuriko Mlimba

Spread the loveMWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk.  Rose Rwakatare...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!