Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Masheikh Uamsho wafanyiwa uchunguzi Hospitali
Habari Mchanganyiko

Masheikh Uamsho wafanyiwa uchunguzi Hospitali

Spread the love

 

MASHEIKH wawili wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), wameanza kufanyia uchunguzi wa afya zao, baada ya kutoka mahabusu, walikosota kwa zaidi ya miaka nane (2012-2021), wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Juzi tarehe 15 Juni 2021, Masheikh hao walitoka katika mahabusu ya Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kuwafutia mashtaka hayo katika Kesi ya Jinai 121/2021, iliyokuwa inawakabili kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Masheikh waliofanyiwa uchunguzi wa afya zao katika Hospitali ya Al-Arahma, Zanzibar, leo Alhamisi tarehe 17 Juni 2021 ni, Sheikh Mselemu Ally Mselemu na Farid Hadi Ahmed.

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Saleh Mbarak Mazrui, amesema Masheikh hao wameshafanyiwa uchunguzi na kwamba mmoja wapo amebainika hana matatizo yoyote.

“Mpaka sasa tumepata watu wawili, tumepima vipimo vyao, mmoja wapo mpaka sasa hana matatizo yoyote. Tunasubiri wengine tuone kama kuna shida yoyote ama hakuna shida yoyote,” amesema Dk. Mazrui.

Dk. Mazrui amesema, ni muhimu Masheikh hao kufanyiwa vipimo kujua hali zao kiafya, kwa kuwa wanatoka kwenye mazingira hatarishi.

“Tunawafanyia vipimo na hii ni muhimu sababu wamekaa vifungoni kwa muda mrefu na maeneo waliyokuwepo ni hatarishi, wamekaa katika sehemu ambayo wako wengi na tunajua sehemu ambayo wako watu wengi , kuna maradhi ya kuambukiza,” amesema Dk. Mazrui.

Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Abdallah Said Ali, amesema waliamua kufika hospitalini hapo, kufanyiwa vipimo ili kubaini hali zao kiafya.

“Leo niko hapa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, baada ya kukaa gerezani kwa muda wa miaka nane. Tukashauriana si vyema kwamba kurejea majumbani mwetu, halafu hatujui afya zetu. Isije kuwa tumeathirika na maradhi yoyote ya kuambukiza,” amesema Sheikh Ali na kuongeza:

“Ikawa yale maradhi unayapeleka nyumbani kwako, badala ya kuathirika mtu mmoja, unaenda kuathiri na watoto, ndugu na mke. Kwa hiyo kuweza kuweka salama familia zetu, tukaamua tuje kufanya vipimo ambavyo vitatuweka sisi kuwa salama.”

DPP Mwakitalu aliwafutia mashtaka Masheikh hao na wengine 16, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kuwafutia mashtaka 14 kati ya 25 yaliyokuwa yanawakabili, kwenye Kesi ya Jinai 121/2021, tarehe 23 Aprili 2021.

Mahakama hiyo ilifuta mashtaka hayo, kwa maelezo kwamba hayakufanyika Tanzania Bara, hivyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa yaliyofanywa visiwani Zanzibar.

DPP Mwakitalu alisema, mashtaka 11 yaliyosalia hayakuwa na nguvu, sababu iliyopelekea ofisi yake kuyafuta.

Masheikh hao wameachwa huru baada ya kusota mahabusu kwa miaka minane, tangu walipokamatwa katika nyakati tofauti kati ya 2012 na 2014.

Katika kesi hiyo, walikuwa wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, walijihusisha na makosa ya ugaidi, kinyume na kifungu cha 27 (c), cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Gardner Habash wa Clouds Fm afariki dunia

Spread the loveALIYEKUWA mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kinachorushwa na kituo cha...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

error: Content is protected !!