January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Masheikh, Maaskofu waonya CCM

Viongozi wa dini walipokutana na Rais Jakaya Kikwete

Spread the love

BAADHI ya viongozi wa madhehebu ya kidini nchini, wameapa kutomuunga mkono mgombea yeyote wa urais anayetafuta urais kwa hongo, hata kama anang’aa kama jua wakati wa mchana na mwezi nyakati za usiku. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu, Sheikhe Athuman Mkambaru, mjini Morogoro juzi.

Masheikh na Maaskofu walitoa kauli hiyo, walikuwa kwenye kongamano la kidini, lililohudhuriwa na viongozi wa madhehebu ya kidini takribani 460, wakiwamo maaskofu, mashekhe na wachungaji.

Viongozi walioshiriki kongamano hilo, ni kutoka mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Kagera, Katavi, Tanga, Mara, Mwanza, Iringa, Njombe, Rukwa, Mbeya, Singida, Dodoma, Ruvuma, Tabora, Unguja, Kilimanjaro, Arusha, Lindi na Mtwara.

Mkumbaru alisema iwapo nchi itaongozwa na mtu anayenunua uongozi atagawa utajiri wa taifa nje, ambapo kwa kipindi hiki Tanzania inataka rais wa kuliponya taifa ambalo kwa kuwa lipo mahututi kwa madeni na rushwa. 

Alisema ni wakati muafaka vijana kote nchini kujithamini na kuacha kutumika kama madaraja ya kuvushia wenye  tamaa  ya madaraka. 

Alisema wengi wanaowania madaraka, wakimaliza kutimiza kile wanachokitafuta, hawaonekani tena.

Alisema, “Ni vema mwaka huu vijana waonesheni okomavu wa kusimamia uwezo wa mtu na siyo chama au dhehebu lake. Nchi hii inahitaji mabadiliko na sio wataka urais kwa rushwa.”

Sheikh Mkambaru hakumtaja anayesema, “mwanasiasa anayetafuta urais kwa njia ya rushwa.”

Hata hivyo, anayetuhumiwa kugawa fedha ili kupata madaraka, ni pamoja na Edward Lowassa, Bernard Membe, Mwigulu Nchemba, Mizengo Pinda na January Makamba.

Alisema kama watanzania hawatakuwa makini na kuzikataa rushwa, watalikabidhi taifa kwa vigogo wa mihadarati, wauaji wa albino na mafisadi na kamwe nchi yetu haitainuka kiuchumi.

Alisema pamoja na Tanzania kugundua gesi nyingi, mafuta na madini mengine yanayogunduliwa kila kukicha, bado matumizi yake hayajazingatia usawa; badala yake, gesi na mafuta hayo yananufaisha kikundi kidogo cha watu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Askofu William Mwamalanga, amevionya vyama vya siasa kuacha mara moja kuwapeleka wagombea wa urais kwenye kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ili kuhiji  wakati kiuhalisia hawana maadili ya mwasisi huyo.

Mwamalanga aliwataka watia nia hao wamkimbilie Mungu na kutubu kwake kwani  yeye ndiye mwenye msamaha kwa kila mwanadamu na siyo Mwalimu Nyerere.

“Kila mtu hapa ana chama chake cha siasa kama yalivyo madhehebu yetu ya kidini, ambapo kila mtu anasema dini yake ni bora kuliko ya mwenzake.   

“Je, umasikini, njaa, rushwa, madhara ya mihadarati na uchafu mwingine ndani ya taifa vimechagua dini, au chama? Mwaka huu ni mwaka wa kupata kiongozi mwenye huruma na wannachi; siyo kiongozi anayejitaza yeye binafsi,” ameeleza.

Wakisoma tamko la  vijana mbele ya maaskofu na mashekhe wanaohudhuria kongamano hilo baadhi  vijana waliomaliza vyuo vikuu vya Sua,  UDOM, UDSM, Tumaini, Teofilo Kisanji, Saut  na Mzumbe, wamekiri kutokuwa na mchango wowote wa kukuza uchumi wa nchi, kupitia sekta za kilimo na elimu.

Vijana hao walitaja sifa tisa ambazo sharti anayetaka kuwa rais wa awamu ya tano, ni lazima awe nazo. Sifa hizo, ni pamoja na kuwa na uwezo  wa  kuwaondolea wananchi kwenye mfumo kandamizi na awe  hajawahi kukataliwa  au kuonywa na viongozi wa nchi au shutuma zozote.

Walitaka mhusika kutojilimbikizia utajiri, kashfa za rushwa, mpenda haki, mwenye uwezo wa kuongoza, mkweli; hajawahi kutorosha fedha nje  ya nchi na  hajaonekana kwa  wapiga ramli ili kutafuta kupendwa  na watanzania.

Baada ya mafunzo hayo, vijana waliamriwa kwenda kote nchini kuelimisha wananchi sifa za Rais ajaye ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa taifa na vizazi vijavyo.

Alitangaza mwaka 2015  kuwa ni mwaka  wa mabadiliko ya kweli kifikira  kwa kuwakata  watoa rushwa hadharani ili haki iwe  wimbo kwa kila mtanzania.

error: Content is protected !!