July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mashabiki wa Simba, Yanga waonywa

Spread the love

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewaonya mashabiki wa Simba na Yanga watakaohudhuria kwenye mechi itakayofanyika kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kufuata sheria na taratibu za usalama ili kuondoa usumbufu, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TFF zilizopo jijini Dar es Salaam leo, Bakari Kizuguto ambaye ni Ofisa Habari wa TFF, amesema, TFF imejipanga kwa kushirikiana na jeshi la polisi kulinda usalama na kwamba atakayebainika kuanzisha fujo jeshi litamshughulikia.

“Mechi za Simba na Yanga huwa ngumu kutokana na baadhi ya Mashabiki wa klabu hizo hukosa ustahimilivu wakati wakishangilia klabu zao zinapocheza hadi kupelekea kuanzisha fujo pindi wanaposhindwa kuelewana,” amesema Kizuguto na kuongeza.

“Kwa kulijua hilo, TFF inawatahazarisha mashabiki wa timu hizo kuwa wastaarabu, kuzingatia sheria na taratibu, atakayeanzisha fujo, safari hii jeshi la polisi limejipanga kuwakabili.”

Kizuguto amewahakikishia mashabiki na wadau wa soka nchini, upatikanaji wa tiketi za kutosha na usalama wake, kwa kuwa safari hii hakuna mianya ya utolewaji wa tiketi feki.

“Safari hii tumetengeneza tiketi imara na madhubuti hakuna atakayetoa tiketi feki, mashabiki wajitokeze kwa wingi kununua tiketi kwenye maeneo yaliyoainishwa na TFF,” amesema.

Kizuguto amekumbushia bei za tiketi hizo kuwa ni Tsh. 7,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, 10,000 machungwa, 20,000 VIP B na 30,000 VIP A, ambapo zitauzwa kwenye vituo kumi ikiwemo kituo cha Oil Com Buguruni na Ubungo, TFF na Uwanja wa Taifa.

Aidha, Kizuguto amesema, mashabiki watakaohudhuria uwanja wa Taifa kuangalia mechi hiyo, ambayo klabu ya Yanga itakuwa mwenyeji ikiikaribisha klabu ya Simba, kutoingia vifaa hatarishi pamoja na vilevi.

“Mashabiki hawaruhusiwi kuingia uwanjani na silaha, vimiminika, vilevi na mabegi yasiyo na ulazima ili kuhakikisha usalama, pia wageni waalikwa wanatakiwa kuja na vitambulisho ili kuondoa usumbufu,” amesema Kizuguto.

Kizuguto ameongeza: “Watakaokuja na watoto wadogo wahakikishe wanawapakata ama kuwakatia tiketi ili kuondoa usumbufu wa upungufu wa siti kwa baadhi ya mashabiki ambapo watoto wadogo wasiokata tiketi hukalia siti hizo kinyume cha sheria.”

Tiketi zimeanza kuuzwa leo mpaka kesho majira ya saa sita mchana.

error: Content is protected !!