October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mashabiki Mbeya City, Simba na Yanga wapigwa ‘stop’

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imetoa zuio la Timu ya Mbeya City kucheza michezo yake ya nyumbani ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) bila mashabiki. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Pia, zuio hilo linazihusu timu za Simba na Yanga katika michezo yake yote itakayocheza nje ya Dar es Salaam.

Hatua hiyo inalenga kujikinga na kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Hayo yalisemwa jana Alhamisi tarehe 25 Juni 2020 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Shamimu Nyaki, Kaimu Mkuu wa Kitengo Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Shamimu alisema, michezo yote iliyobaki ya Mbeya City itachezwa bila mashabiki katika uwanja wa Sokoine kutokana na kukiukwa kwa mwongozo wa afya michezoni wakati wa mchezo kati ya timu hiyo na Simba.

Katika mchezo huo uliofanyika Jumatano ya tarehe 24 Juni 2020, ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa 2-0 na kuendelea kujihakikishia kutetea kombe hilo la VPL kwa msimu wa 2019/20 kwa kufikisha alama 78.

“Pamoja na hatua mbalimbali za kiafya kuzingatiwa, uchunguzi umebaini wawakilishi wa timu mwenyeji na wadau wengine ambao ndiyo walikuwa na dhamana ya kudhibiti mageti, hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo.”

“Badala yake waliruhusu mashabiki wenye tiketi na wasiokuwa na tiketi kuingia uwanjani hovyo na kuharibu mpangilio wa ukaaji kiwanjani,” alisema Shamimu

Katika taarifa hiyo, ilisema hatua hiyo inalenga kuwakumbusha vilabu wenyeji, wasimamizi wa michezo na wadau wengine kote nchini kuendelea kusimamia kikamilifu mwongozo wa afya na taratibu nyingine michezoni hadi hapo Serikali itakapojiridhisha ugonjwa wa COVID-19 umekwisha kabisa nchini humo.

“Hatua hizi zinalenga kuwalinda wananchi, wachezaji weneywe, viongozi na Watanzania kwa ujumla,” imeeleza taarifa hiyo

Shamimu alisema kwa kuwa imeonekana viwanja vingi nje ya Dar es Salaam ni vidogo na wenyeji na wadau wengine wanashindwa kukabiliana na watazamani kuingia uwanjani kwa uchache, ili kufuata masharti ya mwongozo wa afya.

“Wizara inaelekeza michezo yote itakayohusisha timu za Simba na Yanga nje ya Dar es Salaam mashabiki hawataruhusiwa kuingia uwanjani kuangalia mechi zilizosalia isipokuwa tu pale itakapojiridhisha kupitia kamati za ulinzi na usalama za mikoa husika ya klabu mwenyeji,” ilieleza taarifa hiyo

error: Content is protected !!