KUELEKEA mchezo wa fainali wa kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kutazama mchezo huo ni elfu 10 tu, na tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa kuanzia Julai 19 Mwaka huu. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea)
Mchezo huo safari hii utapigwa mkoani Kigoma juali 25 mwaka huu, majira ya saa 9:30 jioni.
Akizungumza jana usiku kupitia kipindi cha michezo cha Wasafi Redio, mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Salum Madadi alisema kuwa “Kwa Uwanja huu hatutoruhusu kuingiza watu zaidi ya 10,000.”
Raia Mwema lilipomtafuta kutaka ufafanuzi zaidi juu ya idadi hiyo ya mashabiki na ukubwa wa mchezo huo, Madadi alisema kuwa hawezi kulizungumza hilo kwa sasa mpaka watakapo kaa kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.
“Tiketi zitaanza kuuzwa tarehe 19 mwezi huu, ila idadi ya kuwa zitauzwa ngapi kwa sasa bado ila tutatangaza, baada ya kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.” Alisema Madadi
Aidha katika upande mwengine wa maandalizi ya mchezo huo, Madadi alisema kuwa mpaka sasa wameshapiga hatua kubwa, hasa kwenye eneo la Uwanja.

“Tupo vizuri na tumepiga hatua kubwa hasa kwenye eneo la kuchezea ‘Pitch’ na miundombinu mingine ya Uwanja na kila kitu kinaenda sawa.” Alinena Mkurugenzi huyo wa mashindano.
Mchezo huo utakuwa wan ne kuwakutanisha wababe hao wawili katika msimu mmoja, katika michezo mitatu iliyopita Yanga ilifanikiwa kushinda miwili ukiwemo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na fainali ya kombe la Mapinduzi sambamba na kwenda sare mechi moja.
Simba inakwenda kucheza mchezo huo huku wakiwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu, na walifuzu fainali hiyo kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, kwenye mchezo wa nufu fainali dhidi ya Azam FC.

Kwa upande wa Yanga wanaenda kwenye mchezo huo, huku wakiwa na rekodi ya kupata matokeo kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba, kwa bao 1-0, na walitinga fainali hiyo mara baada ya kuifunga Biashara United kwa bao 1-0.
Hapa kuna kuvaa barakoa na kuepuka msongamano? Tumewaahidi wafadhili kuwa tutatekeleza maagizo ya wataalamu kuhusu Covid halafu tunapuuza?