JUHUDI za rais wa Marekani, Donald Trump, kuubadilisha muswada wa afya wa Obamacare zinaelekea kugonga mwamba kufuatia baadhi ya viongozi katika chama cha Republican kutokukubaliana na mabadiliko hayo, anaandika Catherine Kayombo.
Kufuatia Trump kushindwa kupitisha muswada huo, tayari Maseneta wawili wa chama cha Republican wamepinga mpango wa chama chao wa kuubadilisha muswada wa Obamacare hatua iliyofanya washindwe kupiga kura ya maoni.
Maseneta hao, Mike Lee na Jerry Morgan walitangaza kwamba hawawezi kuunga mkono mswaada huo, na kwamba kukubaliana nao ni kuidhinisha sera mbaya katika nchi yao.
Mbali na hayo, Maseneta wengine wawili, Rand Paul na Susan Collins wametangaza kuupinga mswada huo wakidai kuwa hautoshi kufuta bima hiyo ya afya.
Mgawanyiko huu unajitokeza ambapo chama cha Republicans kinashikilia viti 52, katika Bunge la Seneti lenye wanachama 100, hali ambayo itakuwa vigumu kuidhinisha mswaada huo.
Maseneta kutoka chama cha Democratic wamesema kuwa hawatakubali kubadilisha mswaada huo wa Obamacare, lakini kwa kushirikiana na wanachama wa Republican wanaweza kufanya kazi kwa pamoja ili kuufanya uwe imara.
Rais Donald Trump, aliahidi kubadilisha muswada huo kama ahadi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, ikiwa ni namna mojawapo ya kubadilisha mfumo wa uongozi.
Leave a comment