KIONGOZI mwandamizi klabu ya soka ya Simba ya Tanzania, Marco Masanja, aliyekuwa kifungoni nchini China, amefariki dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Masanja aliyepata kuwa katibu mkuu msaidizi na makamu mwenyekiti wa klabu hiyo miaka kadhaa huko nyuma, alifariki dunia tarehe 10 Februari mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizofikia MwanaHALISI Online, kutoka kwa mmoja wa wanafamilia wa mwanamichezo huyo zinasema, Masanja alifariki dunia kutokana na maradhi ambayo hayakutajwa.
Kiongozi huyo wa zamani wa Simba, alikamatwa nchini China, akituhumiwa kusafirisha madawa ya kulevya. Alihukumiwa mwaka 2013, kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.
Taarifa zinasema, alitarajiwa kumaliza kifungo chake, mwaka 2025.
“Ni kweli kwamba ndugu yetu, kaka yetu, baba yetu na mwanafamilia wetu, Marco Masanja, amefariki dunia akiwa anatumikia kifungo chake nchini China,” ameeleza Salum Malilima, mmoja wa wanafamilia wa marehemu.
Anaongeza, “hatufahamu mazishi yake yatafanyika lini. Lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa marehemu atazikwa huko huko China kwa sababu ya ukubwa wa gharama za kuusafirisha mwili wa kuja Tanzania.”
Wakati wa uhai wake, Marco Masanja alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Simba, ikiwa ni pamoja na katibu mkuu msaidizi chini ya Kassim Dewji na makamu mwenyekiti wa timu hiyo.
Aidha, kabla ya kutiwa mbaroni, Masanja alikuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kata ya Kiwalani, wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salam.
Alikamatwa katika mji wa Guangzhou, akituhumiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kula njama, kusambaza na kusafirisha madawa ya kulevya. Serikali ya China, imeweka sheria kali kwa watu wanaopatikana na makosa ya aina hiyo.
Leave a comment