December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maridhiano ndo chachu ya uchumi Zbar – Mwinyi

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema jukumu muhimu la kuipatia nchi uchumi mzuri, halitafanikiwa iwapo hakuna amani na utulivu katika nchi. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea). 

Hapohapo, akasema amani inahitaji kuwepo kwa maridhiano ya kweli, umoja na mshikamano kwa wananchi na washirika wote.

Rais wa Zanzibar amesema hayo leo katika hotuba fupi aliyoitoa Ikulu mjini hapa mara baada ya kupokea taarifa ya Kikosi Kazi alichokiunda mwezi uliopita baada ya mkutano wa siku tatu wa kujadili mustakabali wa Zanzibar kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Kisauni, uliandaliwa na ofisi yake kwa lengo la kutafuta njia ya kuijengea Zanzibar mifumo ya kuchagiza ukuaji wa demokrasia kama nyenzo ya kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Baada ya mkutano huo uliokusanya wanasiasa, asasi za serikali na za kiraia, taasisi na viongozi wa dini, Rais alimteua Daktari wa Sheria, Ali Ahmed Uki kuongoza kikosi kazi cha kufanya uchambuzi wa maoni yalitotolewa mkutanoni na kuandaa ripoti ya mapendekezo wakitumia pia rejea za Katiba, Sheria za Uchaguzi Tanzania na Zanzibar na ya Usajili wa Vyama vya Siasa Tanzania.

Hafla ya leo ndio ya kukabidhiwa ripoti aliyoelekeza kupatikana ndani ya siku 15.

Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais ya Mapinduzi Zanzibar, akiapa mbele ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi Ikulu Zanzibar

Akiwasilisha ripoti, Dk. Uki ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Zanzibar University) alieleza baadhi ya mapendekezo ni kutaka kutungwa sheria mahsusi ya Tume ya Pamoja ya Fedha – Joint Finance Commission (JFC) ili kuwezesha kutekelezwa kwa maazimio yaliyo kwenye ripoti ya Tume hiyo iliyoundwa wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa kutafuta mfumo wa mgawanyo wa mapato na matumizi ya Serikali ya Muungano.

Tume hiyo iliazimia utaratibu wa uendeshaji serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotokana na kuunganishwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar katika Muungano ulioasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964.

Mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti aliyokabidhiwa Rais Dk. Mwinyi yakiwemo masuala mahsusi yanayoihusu tu Zanzibar, yanatarajiwa kujumuishwa kwenye maoni ya ripoti ya Kikosi Kazi alichokiunda Rais Samia Suluhu Hassan.

Mbali na Dk. Uki, walioteuliwa kuunda kikosi kazi na Rais Mwinyi, ni Balozi Amina Salum Ali, Prof. Makame Ussi, Vuai Ali Vuai, Ismail Jussa Ladhu, Ameir Hassan Ameir, Joseph Abdalla Meza, Said Mohamed Mzee, Rukia Ahmed, Rev Stanely Nicholas na Thabit Norman Jongo.

error: Content is protected !!