July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Marekebisho ya sheria: Wanahabari walilia uhuru, maslahi

Spread the love

 

IKIWA vuguvugu la marekebisho ya sheria zinazosimamia sekta ya habari likizidi kuongezeka nchini Tanzania, wanahabari wamepaza sauti zao kuhusu uboreshwaji wa uhuru wa kufanya kazi na maslahi yao. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wakizungumza katika nyakati tofauti na MwanaHALISI Online, wanahabari hao wameiomba Serikali iboreshe sheria hizo ili kuhakikisha vifungu vinavyominya uhuru wa kupata, kutafuta na kutoa habari, vinaondolewa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Selemani Msuya, ameshauri mfumo wa upatikanaji habari uboreshwe, kwa kuondolewa vifungu vya sheria vinavyotoa mamlaka kwa watendaji wa Serikali kuwapangia wanahabari aina za maudhui ya kutoa.

Wakati huo huo, Msuya alishauri maslahi ya waandishi wa habari yaboreshwe, ikiwemo kwa kupewa mikataba na mishahara.

“Suala zima la uhalisia wa habari unaanzia katika mfumo wa kutafuta habari na maisha gani ya wanahabari. Mfano waandishi wa habari wengi hawana mikataba, wanakosa stahiki zao kama bima ya afya na mafao wanapostaafu. Pia, hutoi kodi kwa Serikali sababu unalipa posho haukatwi hausaidii nchi kuendelea,” amesema Msuya na kuongeza:

“Sheria zirekebishwe, zitamke mwajiri iwapo umemtaka mtu ndani ya utumishi wake isizidi miezi sita apewe mkataba wa kudumu.”

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekinolojia

Kwa upande wake, Mwanahabari kutoka Wasafi Redio, Charles William, ameshauri sheria irekebishwe ili jukumu la kuadhibu vyombo vya habari vinavyofanya makosa liwe la mahakama na si Idara ya Habari Maelezo kwa magazeti na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa vyombo vya kielektroniki.

“Kuna maeneo nadhani hayako sawa, ni sehemu ambazo sheria zimeweka mamlaka kwa watu, mfano kwenye magazeti kuna Idara ya Habari Maendeleo, kupitia mkurugenzi. Wanayo mamlaka kusimamisha uchapishaji wa chombo cha habari chochote ambacho kinaandika maudhui ambayo hawayapendi,” amesema William na kuongeza:

“Kwa upande wa Televisheni na redio, haipaswi TCRA kupewa mamlaka ya kukifungia chombo badala yake kama itaona kuna redio ambayo inatoa maudhui ambayo yanakiuka kanuni au sheria, basi wanmatakiwa kushitaki chombo hicho mahakamani ili isikilize pande zote mbili iamue kama kweli imefanya makosa.”

Mwandishi wa Mwanzo TV, Asia Gamba, naye amependekeza “maoni yangu ni kwamba, kipengele cha uhuru wa habari kiongezeke. Hivi sasa tunaambiwa kuna uhuru lakini bado haujitosheleze. Tanzania tunao wanahabari wengi wanapatiwa vikwazo vya hapa na pale.”

“Kimsingi kutokuwepo kwa uhuru wa habari kunasababisha weledi wa wanahabri kudhoofika hivyo katika kipengele hicho naona uhuru wa habari unapaswa kuongezwa,” amesema Asia.

Mwanahabari kutoka MwanaHALISI Online, Faki Ubwa, amesema “waandishi turuhusiwe kuripoti moja kwa moja kinachoendelea mahakamani katika mienendo ya mashauri yote yenye maslahi mapana ya nchi kama ambavyo jirani zetu Kenya wanavyoruhusu.

“Mahakama inatakiwa kutengua kanuni iliyojiwekea kwani hakuna sababu za kuendesha mashtaka kizani ikiwa magazeti na mitandao inaandika.”

Ubwa ameshauri vikwazo kwa waandishi wa habari wanaoripoti habari za dharura viondolewe.

“Pia nashauri kuondoshwa vikwazo vyote vinavyomchelewesha mwanahabari kuripoti tukio la dharura kama ajali ifiki pahala mwanahabari awe chanzo cha kuaminika stori kwa mfano, ajali imetokea na waziwazi watu kadhaa wamejeruhiwa mwanahabari asiwekewe kikwazo cha kuripoti stori hiyo kwa kuwa Mamlaka haijathibitisha,” amesema.

Mwanahabari kutoka Watetezi Tv, Hilda Ngatunga, ameipongeza Serikali kwa kufungua milango ya marekebisho hayo, akisema itasaidia kuwapa uhuru waaandishi wa habari kuibua habari zenye maslahi mapana kwa Taifa.

“Marekebisho haya ya sheria mbalimbali hasa za habari yamefungua wigo wa uhuru wa kujieleza. Jamii pamoja na vyombo vya habari vitaweza kuhoji, kutafuta na kuchakata habari bila kuingiliwa.

“Pia itarudisha moyo kwa wanahabari kutafuta habari zenye kuibua masuala ya uonevu na yanayovunja haki za binadamu bila woga wa kufungiwa ama kupotezwa,” amesema Hilda.

error: Content is protected !!