June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Marekani yajitosa sakata la Mbowe, Tanzania yajibu

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

KAMATI Ndogo ya Mambo ya Nje ya Afrika ya Baraza la Wawakilishi nchini Marekani, imeiomba Serikali ya Tanzania, imuache huru Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema, Freeman Mbowe, anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe anatuhumiwa na Polisi kupanga njama za mauaji ya viongozi wa serikali pamoja na ugaidi.

Wito huo umetolewa jana Alhamisi, tarehe 22 Julai 2021 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Karen Bass, saa kadhaa baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa ya kumshikilia Mbowe, kwa ajili ya mahojiano kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Katika taarifa yake, Karen anavitaka vyombo vya dola kumwachia huru Mbowe akiwa salama mwenye afya njema.

Mbowe pamoja na wanachama wengine 11 wa Chadema, walikamatwa jijini Mwanza na Jeshi la Polisi, saa 8 usiku wakiwa katika Hotel ya Kingdom tarehe 21 Julai 2021.

Karen Bass, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mambo ya Nje ya Afrika ya Baraza la Wawakilishi nchini Marekani

Walikamatwa saa chache kabla hawajafanya kongamano la kudai katiba mpya, jijini humo. Hata hivyo, halikufanyika baada ya kujikuta wakiishia mikononi mwa dola.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mwanza, Mbowe baada ya kuhojiwa kwa tuhuma hizo, alisafirishwa hadi Dar es Salaam, kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kufuatia tuhuma zinazomkabili.

Akizungumzia tukio hilo, Karen ametoa wito kwa mamlaka za Tanzania, kuacha kuwakamata wanasiasa wa upinzani.

Amesema, mara baada ya kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, walikuwa na matumaini kwamba ataibadili nchini.

“Nimesikitishwa kusikia kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Tanzania, Mbowe, wafanyakazi na wanachama wengine 11, ambao ni sehemu ya maendeleo ya demokrasia,” amesema Karen.

“Mamlaka za Tanzania lazima zimalize ukandamizaji unaozidi kuongezeka wa vyama vya upinzani na viongozi. Kuwakamata watu kinyume cha sheria na kuwaweka kizuizini kunaonesha upuuzwaji wa sheria, haki za binadamu na haki ya kujieleza na kushirikiana,” amesema.

Gerson Msigwa, Mkuu wa Idara ya Habari na Maelezo

Amesema tukio hilo linapunguza matumaini dhidi ya ustawi wa misingi ya demokrasia na utawala bora Tanzania.

“Rais Samia alipoingia madarakani alionekana kuwa tofauti, katika kuiongoza Tanzania kuelekea jamii yenye demokrasia. Kwa bahati mbaya kukamatwa kwa Mbowe na viongozi wa upinzani kunapunguza matumaini hayo,” amesema Karen.

Marekani inaungana na mashirika ya ndani na nje ya Tanzania yanayotetea haki za binadamu kukosoa vikali hatua hiyo ya jeshi la polisi, kuwakamata usiku wa manane.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), na Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu Amnesty International, Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Ulimwenguni (IDU) na Taasisi ya Muungano wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA), ni miongoni mwa waliojitokeza kupinga kukamatwa kwa Mbowe na wenzake.

Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa akihojiwa leo Ijumaa, tarehe 23 Julai 2021 na kituo cha Wasafi kuhusu matamko hayo amesema, kila nchi zina taratibu zake “tuliachie jeshi la polisi lifanye kazi yake, likimaliza litatueleza.”

Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo amesema, matamko hayo hayawezi kuzuia uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili mtu yoyote huku akiwataka wananchi kuwa watulivu wakati suala hilo likiendelea kufanyiwa kazi.

error: Content is protected !!