August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Marekani yaiasa Z’bar

Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman

Spread the love

MAREKANI imeipa nasaha Zanzibar kuendeleza moyo wa maridhiano ya kisiasa kwa kuamini kuwa ni fursa nzuri ya kuimarisha umoja na mshikamano ambao ni muhimu katika kuchagiza maendeleo ya watu. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea). 

Nasaha hizo zimetolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright wakati alipokutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ofisini kwake eneo la Migombani mjini Zanzibar.

Balozi Wright aliyefika ofisini kwa Makamu wa Kwanza kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa – Government of National Unity (GNU) – amesema umoja na mshikamano wa kitaifa katika nchi huwapa ubalozi ari na moyo wa kushawishi serikali yao pamoja na wafanyabiashara wa Marekani kuja kuwekeza nje.

“Maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar ni fursa ya watu wote kuwa pamoja, kusahau tofauti zao za itikadi za vyama na ikifika hapo, Marekani haitowacha kutumia mlango huo kuvuta wawekezaji huku serikali nayo ikifikiria kuongeza fungu la misaada yake, zikiwemo fedha za kuwajengea vijana ujuzi ili wajikite katika shughuli za kilimo na ujasiriamali,” alisema.

Balozi Wright ambaye amefuatana na ofisa mwandamizi wake wa masuala ya siasa, Kristin Mencer, amesema Marekani inajikuta na wajibu wa kuunga mkono serikali ya Zanzibar katika jitihada zake za kuwaletea watu wake maendeleo endelevu.

Awali Balozi Wright alimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais Othman akisema wakati wote imekuwa ni imani yake kuwa mazingira tulivu ya kisiasa hujenga mshikamano wa kitaifa kwa jamii na kuwa nyenzo kuu ya nchi kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi.

Ametaja hatua anazozichukua Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan za kuunda Kikosi-Kazi cha kuratibu Mabadiliko ya Katiba na kitendo cha hivi karibuni cha kufika kisiwani Pemba na kukutana na viongozi mbalimbali wa kisiasa, akisema ni ishara nzuri kwani “Pemba ndiko kwenye wahanga wakuu wa siasa mbaya.”

“Tunabaini sasa dhamira ya utekelezaji mapendekezo yanayotoa mwangaza wa kujenga maridhiano na umoja wa kitaifa katika ngazi tofauti. Sisi kama kawaida yetu, tuko tayari kushirikiana kwa lengo la kufanikisha maridhiano ya kitaifa yaliyo endelevu,” alisema.

Makamu wa Kwanza wa Rais alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ni sehemu nzuri kwa viongozi wakuu kuanzia katika kutimiza dhamira ya kuleta mabadiliko makubwa katika nchi kiuchumi na kuimarisha huduma za kijamii.

Serikali ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi inaundwa na vyama vya CCM na ACT – Wazalendo vilivyopata kura za kukidhi kigezo cha kikatiba cha kushirikiana kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa 2020.

error: Content is protected !!