May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Marekani yafanya ‘uchochezi,’ yawaonya wanaokuja Tanzania

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam 'Terminal 3'

Spread the love

 

SERIKALI ya Marekani nchini Tanzania, imeonya wasafiri wanaotaka kutembelea taifa hilo kutofanya hivyo, kufuatia kuwapo kwa maambukizi makubwa ya virusi vya Corona. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Marekani nchini imeeleza kuwa pamoja na serikali ya Tanzania haijatoa takwimu zozote tangu Aprili mwaka jana, “lakini ya virusi hivyo, bado ni makubwa.”

Marekani inasema, kwa kipindi chote cha mlipuko wa Corona, taifa hilo la Afrika Mashariki, halijapiga marufuku ya raia wake kutoka nje, lakini pia haijachukua hatua nyingine, ikiwamo kutoa miongozo ya namna bora ya mikusanyiko na matumizi ya usafiri wa umma.

Kwa mujibu wa ubalozi huo, huenda hospitali na vituo vya afya vikazidiwa na wagonjwa kutokana idadi kubwa ya watu kuambukizwa virusi vya Corona nchini; upimaji wa virusi hivyo siyo wa uhakika.

Ubalozi unasema, mashaka yake yanatokana na baadhi ya wale waliopimwa na kupatiwa vyeti vya kuonyesha hawana maambukizi, walipopimwa kwenye mataifa mengine, walibainika kuwa na virusi hivyo.

Onyo hili la Marekani linakuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kusema, serikali yake haijamzuia mtu yeyote kuvaa barakoa, japo anashauri matumizi ya barakoa zilizotengenezwa nchini mwake.

Amesema, anaamini baadhi ya zile zinazoagizwa kutoka nje, siyo salama. Alitoa kauli hiyo, Jumapili iliyopita, jijini Dar es Salaam.

Kauli yake hiyo, imeonekana kama imebadili msimamo wake kuhusu ugonjwa wa Covid 19.

Huko nyuma, kiongozi huyo alisikika akibeza matumizi ya barakoa kwa maelezo kuwa nchi yake, imefanikiwa kutokomeza maambukizi ya Corona.

Aidha, Rais Magufuli amekuwa akieleza kutokuwa na imani na chanjo ya Corona, inayotolewa ulimwenguni. Amewalaumu hata baadhi ya watu waliokwenda ng’ambo na kupatiwa chanjo na ”kurejea na Corona ya ajabu ajabu.”

Amesema, “vita ya uchumi ni kubwa na ni mbaya,” hivyo ametaka raia wa Tanzania kusimama imara na kumtanguliza Mungu mbele kwani hakuna linaloshindikana kwake iwapo watamuomba kwa uaminifu.

Ameagiza siku tatu za maombi ambapo aliwataka waumini wa dini zote, kufunga na kusali kuliombea taifa dhidi ya virusi vya corona. Hii ni mara ya pili rais Magufuli kutaka wananchi wake kuomba dhidi ya Corona.

Mapema mwaka jana, wakati maambukizi ya virusi hivyo yalipokuwa yamepamba moto kote ulimwenguni, Rais Magufuli aliwataka wananchi kutokuwa na hofu, badala yake wamtangulize Mungu mbele kwa kusali.

Baadae akasikika akitangaza kuwa taifa limeishinda Corona, kauli ambayo ameendelea kuishikilia na kuisisitiza, wiki iliyopita ambapo alisema, “kama mwaka jana tulishinda na mwaka huu tutashinda.”

Hatua ya Ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari kwa wasafiri wanaotaka kukuja nchini, imekuja wakati kituo cha kupambana na magonjwa nchini humo, kimeelekeza watu kutosafiri nchini Tanzani.

Kituo hicho kimesema, licha ya taifa hilo, kusema liko salama, kutokana na kutumia njia mbambali za asili ikiwemo kujifukiza na hata matumizi mimea na matunda, lakini kasi ya maambukizi bado ni kubwa.

Tanzania haijatoa takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona, tokea Aprili mwaka jana.

Siku kadhaa zilizopita, Serikali ya Oman nayo ilipiga marufuku wasafiri kutoka Tanzania kuingia nchini humo, marufuku ambayo inatarajiwa kudumu kwa muda wa siku 15.

Habari kutoka Oman zinasema, hatua hiyo imetokana na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya udhitibi wa Corona nchini humo.

Kamati hiyo imewataka wananchi wa Oman kutosafiri nje ya nchi ili kuzuia maambukizi na ikibidi kusafiri basi kuwe na sababu maalum.

Marufuku hiyo inatarajiwa kuathiri sehemu kubwa wasafiri kutoka Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa kuna watu wengi wanaosafiri kila siku kuelekea Oman, kutokea Tanzania.

error: Content is protected !!