July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Marando: Wezi wa Escrow wamefichwa na Ikulu

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando

Spread the love

MABERE Nyaucho Marando, wakili mashuhuri nchini na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anasema, “…pamoja na kujiuzulu kwa Prof. Sospeter Muhongo, bado ukweli kuhusu wizi katika Akaunti ya Tegeta Escrow, unahitajika.”

Amesema, “Kujiuzulu pekee hakutoshi. Ni lazima umma ufahamishwe , nani aliyeiba fedha za umma; wapi zimewekwa; zinatumikaje na nani aliyeruhusu wizi huo kutendeka.” Anaadika Saed Kubenea… (endelea).

Akizungumza kwa uchungu Marando amesema, kujiuzulu pekee hakutoshi. Ni sharti wahusika wote wakuu wa wizi huu, wahojiwe na kukamatwa.”

Fedha katika akaunti ya Escrow zilikwapuliwa kati ya Oktoba na Novemba mwaka 2013. Akaunti ya Escrow ilifunguliwa kutokana na kuibuka kwa mgogoro kati ya Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Mgogoro huu wa uwekezaji kati ya Tanesco na IPTL ulitokana na kuwapo madai ya udanganyifu yaliyofanywa na IPTL, katika gharama za uwekezaji; uwekaji wa mitambo na nyumba za wafanyakazi.

Lakini Marando anasema, “…wizi huu ulianzia Ikulu na umefanyika kwa baraka za Ikulu na mbele ya macho ya Rais Jakaya Kikwete. Umewashirikisha baadhi ya maofisa wa ndani wa Ikulu na hata familia yake imetajwa.”

Anasema, ushahidi kuwa rais anahusika na wizi huu, ni barua ya 14 Novemba 2013, iliyoandikwa na katibu mkuu wizara ya fedha.

Barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Likwalile iliwasilisha kwa gavana wa BoT, Prof. Benno Ndulu kwa ajili ya utekelezaji, kile anachoita, “maagizo ya Rais Kikwete.”

Katika barua hiyo, Dk. Likwalile ameelekeza fedha katika akaunti ya Escrow zilipwe kwa kampuni ya PAP. Dk. Likwalile alikuwa akirejea maagizo kutoka kwa Rais kwa barua ya tarehe 13 Novemba 2013. Ilisainiwa na Katibu wa Rais, Prosper Mbena.

Anasema, hatua madhubuti za kushughulikia ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, hazijakamilika na haziwezi kukamilika bila kuhojiwa au kuwajibishwa kwa Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndullu, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Katibu Mkuu wizara ya Fedha, Dk. Dk. Servacius Likwalile na maofisa wa ikulu na hata rais mwenyewe ambaye ndiye aliyeruhusu fedha hizo kutolewa.

Akirejea kauli mbalimbali za serikali, Marando anasema, kwa kipindi chote hicho, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, huku akijua yote yaliyotendeka, aliendelea kusisitiza kuwa serikali ilitekekeza wajibu wake kikamilifu katika jambo hili, wakati haikuwa hivyo.

“Ukweli ni kuwa fedha katika akaunti ya Escrow ziliibwa wakati Pinda na Kikwete wakijua kila kitu na kukibariki,” ameeleza.

Makubaliano kati ya serikali na IPTL siyo tu hayakupata baraka za Bunge, bali hayakupitia hata katika baraza la mawaziri. Hakuna kumbukumbu zozote za serikali zinazoonyesha baraza la mawaziri liliridhia fedha hizo kutolewa na kwamba PAP walipewa fedha hizo wakiwa siyo wamiliki halali wa IPTL.

Anasema, serikali inawafungulia mashitaka waliopewa fedha na James Rugemalira ambazo zimetokana na mauzo ya hisa zake katika IPTL na kuwaacha waliotumia madaraka yao vibaya na kisha kuchota mamilioni ya dola kutoka Benki Kuu na kuzipeleka benki ya Stanbic, kinyume na makubaliano ya serikali na IPTL ya tarehe 21 Oktoba 2013.

Mkataba huo uliagiza fedha hizo zilipwe kupitia akaunti Na. 010-0016-0 na 060-0016-7 zilizoko katika benki ya UBL, tawi la Tanzania.

Lakini fedha hizo zilipelekwa Stanbic na gavana wa BoT kwa maagizo ya Harbinder Sethi Singh; aliyekutana na Rais Kikwete Ikulu na kutoka hapo akachotewa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow.

Akizungumza kwa kujiamini, Marando anasema, “Zipo taarifa kuwa fedha hizi zilichukuliwa kwa maelekezo ya Rais Kikwete kwa lengo la kukisaidia CCM kufanikisha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Hata hivyo, tumeambiwa na watu walioko karibu na chama hicho, kwamba ni sehemu ndogo sana ya fedha hizo iliyofikishwa CCM. Nyingi ya fedha hizo zimechukuliwa na familia ya Rais Kikwete. Ninazo taarifa kuwa familia ya Rais Kikwete imepata zaidi ya Sh. 9 bilioni kutoka fedha za Escrow.”

Anasema, kwa kuwa Bunge limejiridhisha kwamba benki ya Stanbic Ltd., ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP; na hadi sasa hakuna mhusika hata mmoja aliyekamatwa kutoka katika orodha ya walionufuika na wizi huo; na wala hawajatajwa, basi ni jukumu la umma kuhakikisha wote walioshiriki katika wizi huu wanatajwa na kufikishwa mahakamani.

error: Content is protected !!