Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari Marais tisa wamuaga Dk. Magufuli
HabariTangulizi

Marais tisa wamuaga Dk. Magufuli

Mjane Mama Janeth Magufuli akiaga mwili wa mume wake hayati Dk. John Magufuli
Spread the love

 

MARAIS tisa katika nchi za Bara la Afrika, wameshiriki shughuli ya kitaifa ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Shughuli hiyo ya mazishi ya kitaifa ya kuuaga mwili wa Hayati Magufuli, imefanyika leo Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dodoma na kuongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Hayati Magufuli alifariki dunia Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.

Marais waliohudhuria ni; Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (EAC), Filipe Nyusi wa Msumbiji, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Felix Tshisekedi wa Congo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya

Wengine ni; Lazarus Chakwera (Malawi), Azali Assoumani (Comoro),
Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Edgar Lungu (Zambia), Mokgweetsi Masisi (Botswana) na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Pia, kulikuwa na waliowawakilisha wakuu wa nchi, wakiwemo, Makamu wa Rais Burundi, Prosper Bazombana, Makamu wa Rais Namibia, Dk. Nangolo Mbumba, Waziri Mkuu Rwanda, Edourdo Ngirente, Waziri wa Mambo ya Nje Angola, Tete Antonio, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Richard Kabonero.

Mbali na viongozi hao, shughuli hiyo ilihudhuriwa na wawakilishi mbalimbali wa jumuiya za kimataifa, mabalozi na watu mashuhuri.

Akizungumzia ujio wa viongozi hao wa kimataifa, Rais Samia amesema unadhihirisha Hayati Rais Magufuli alikuwa kipenzi cha watu wengi.

Felix Tshisekedi Rais wa Congo

“Hayati Rais Magufuli alikuwa kipenzi cha wengi, inadhihirishwa na uwepo wa wakuu wa nchi wa serikali na wa kikanda na kimataifa, wameshiriki kumuaga ukizingatia wana majukumu yao nchini mwao na nyakati hizi tulizo nazo kusafiri nje ya nchi si jambo rahisi au jepesi lakini wamechukua uzito huo,wamekuja,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewashukuru viongozi hao ambao wote wamemwakikishia ushirikiano akisema “nitumie fursa hii kuwashukuru kwa kufika kwenu, mmetugusa sana, mmetupa heshima sana, tutakumbuka wema wenu huu siku zote.”

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Hayati Rais Magufuli, amesema ujio wa viongozi hao umeleta faraja kwa Watanzania.

“…tuna faraja ya kukimbiliwa na mjirani zetu, tunashukuru sana. Kupata marais tisa walioacha shughuli zao kwenye nchi zao sio ndogo, kupata makamo wa rias wawili kutoka katika nchi zao si jambo dogo, tunawashukuru,” amesema Majaliwa.

Rais wa Zambia, Edgar Lungu

Enzi za uhai wake, Hayati Rais Magufuli alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuanzia 2016 hadi 2017 na mwaka 2019 hadi 2020, alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

Mbali na viongozi wa kimataifa waliohudhuria mazishi hayo, viongozi wa kitaifa waliohudhuria ni, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Prof. Ibrahim Juma.

Dk. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Wengine ni, Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Othman Masoud Othuman, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Othman Makungu.

Vile vile, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, mawaziri na manaibu waziri walihudhuria shughuli hiyo.

Marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassani Mwinyi na Jakaya Kikwete nao wamehudhuria mazishi. Marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mohamed Gharib Billali, nao walikuwapo.

Mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania waliokuwepo ni; Jaji Joseph Warioba, John Malecela, Mizengo Pinda na Frederick Sumaye.

Leo ni siku ya tatu kwa mwili wa Hayati Rais Magufuli kuagwa, ambapo ulianza kuagwa mkoani Dar es Salaam kwa siku mbili, Jumamosi hadi Jumapili tarehe 21 Machi 2021, kwenye Uwanja wa Uhuru mkoani humo.

Emmerson Mnangagwa Rais wa Zimbabwe

Baada ya shughuli hiyo ya kitaifa ya kuuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli kufanyika jijini Dodoma, kesho Jumanne tarehe 23 Machi 2021, utaagwa na wananchi wa Zanzibar, kisha utasafirishwa mkoani Mwanza kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo kutoa heshima zao za mwisho Jumatano tarehe 24 Machi 2021.

Familia ya Hayati Rais Magufuli na wakazi wa wilaya ya Chato mkoani Geita alikozaliwa, watauaga mwili huo Alhamisi tarehe 25 Machi 2021.

Na hatimaye utapumzishwa katika makao yake ya milele wilayani humo Ijumaa ya tarehe 26 Machi 2021.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!