May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Marais 10 Afrika kumuaga Magufuli

Spread the love

 

MARAIS 10 wa Barani Afrika wanatarajiwa kuhudhuria shughuli ya kitaifa ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli (61), itakayofanyika kesho Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili tarehe 21 Machi 2021, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, wakati anazungumzia maandalizi ya shughuli hiyo ya kitaifa ya kuuaga mwili wa Hayati Magufuli.

Magufuli alifariki dunia Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu kwa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Dk. Hassan Abbas, Msemaji wa Serikali

“Kama ambavyo tumesema, msiba huu sio wa Tanzania tu, umegusa dunia nzima na kesho tunatarajia viongozi mbalimbali wa kimataifa watashirikiana nasi kuja kuomboleza kumuaga rais wetu.’’

“Mpaka sasa marais na waowakilisha 11 , jumuiya za kimataifa, mabalozi, asasi za kikanda watakuwa zaidi 50 wamethibitisha kuja,” amesema Dk. Abbasi.

Msemaji huyo wa Serikali ya Tanzania, amewataja marais hao ni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Lazarus Chakwera (Malawi), Azali Assoumani (Comoro), Filipe Nyusi (Msumbiji), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe).

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji

Wengine ni, Edgar Lungu (Zambia), Hage Geingob (Namibia), Mokgweetsi Masisi (Botswana), Felix Tshisekedi (Congo) na Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini).

Mbali na marais hao, Dk. Abbasi amesema Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Rais wa Angola, Joao Lourenco na Rais wa Burundi, Everist Ndiyashimiye, watawakilishwa katika shughuli hiyo.

Hali kadhalika watu zaidi ya 50 kutoka katika jumuiya za kimataifa, ofisi za mabalozi na asasi za kikanda wanatarajiwa kushiriki pia.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli utaagwa kesho Dodoma, baada ya kuagwa mkoani Dar es Salaam kwa muda wa siku mbili (Jumamosi na Jumapili).

Baada ya mwili wa Hayati Magufuli kuagwa Dodoma, tarehe 23 Machi 2021, utaagwa na wananchi wa Zanzibar, kisha utasafirishwa kuelekea mkoani Mwanza, ambapo utaagwa pia tarehe 24 Machi mwaka huu.

Tarehe 25 Machi 2021, mwili huo utaagwa na familia ya Hayati Rais Magufuli na wananchi wa Wilayani Chato mkoani Geita.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli utapumzishwa kwenye makao yake ya milele nyumbani kwao Chato, Ijumaa tarehe 26 Machi 2021.

error: Content is protected !!