October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mapokezi ya Lissu yalivyotikisa

Spread the love

UJIO wa Tundu Antiphas Lissu, makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, umetikisa viunga vya Jiji la Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu amewasilia saa 7 mchana wa leo Jumatatu tarehe 27 Julai 2020 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam akitokea nchini Ubelgiji.

Mwanasiasa huyo amerejea Tanzania baada ya kuwa ughaibuni tangu tarehe 7 Septemba 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari katika makazi yake Dodoma.

Siku hiyohiyo usiku, alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu hadi tarehe 6 Januari 2018 alipohamishwa tena kwenda nchini Ubelgiji hadi leo aliporejea.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema (katikati) akiwasili uwanja Ndege JK Nyerere. Kushoto Freeman Mbowe na John Mnyika (kulia).

Mamia ya wanachama wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki walifika kumpokea Lissu katika uwanja huo wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Alute Mughwai, kaka wa Lissu.

Baada ya kuwasilia na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kukamilisha taratibu, Lissu alitoka ndani akiongozana na Mbowe pamoja na Mnyika, hali iliyoibua shangwe kutoka kwa wale waliofika kumpokea.

Wapenzi wa Chama cha Chadema wakiwa nje ya uwanja wa Ndege wa JK Nyerere

Msafara wa zaidi ya magari 30 na pikipiki, zilianza kutoka uwanjani hapo kwenda Ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufupi, Kinondoni wakipita Tanzania- Buguruni – Amana- Boma – Kigogo – Magomeni – Morocco – Mkwajuni – Studio hadi ofisini hapo.

Iliuchukua takribani zaidi ya saa tatu kutoka uwanjani hapo saa 8 mchana kufika ofisini kwani ulikuwa unakwenda taratibu kutokana na wafuasi waliokuwa mbele ya msafara wakitembea huku wakiusimamia ili kumpa fursa Lissu kuwasalimia wananchi waliokuwa wamesimama barabarani.

Mara kadhaa Lissu alisikika akisema ‘Mungu ni mwema’ huku baadhi wakiimba rais, rais, rais na wengine wakionyesha yuso za tabasamu.

Kuitwa rais, inatokana na Lissu kuwa miongoni mwa watia nia wa urais wa Tanzania ndani ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

error: Content is protected !!