Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mapingamizi ya kina Mbowe yaendelea kutupwa
Habari za SiasaTangulizi

Mapingamizi ya kina Mbowe yaendelea kutupwa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, imekubali kupokea kitabu cha kumbukumbu za mahabusu cha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, kama kielelezo cha jamhuri. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya, Halfan Hassan Bwire na Adam Kasekwa.

Mahakama hiyo imepokea kitabu hicho leo Jumatatu, tarehe 22 Novemba 2021, mbele ya Jaji Joachim Tiganga, akitoa maamuzi madogo ya mapingamizi ya mawakili wa utetezi, wakiomba kisipokelewe kwa madai kielelezo hicho kilishatolewa uamuzi mahakamani hapo.

Mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya walitoa hoja tatu za kisheria, za kupinga upokelewaji wake ikiwemo, kielelezo hicho hakijatolewa kwa amri ya mahakama kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Huku hoja nyingine ikiwa ni, mahakama hiyo kuzuiwa kuijadili na au kukitolea uamuzi kielelezo hicho kwa madai kilishawahi tolewa na kufanyiwa maamuzi na mahakama hiyo.

Jaji Tiganga ametupilia mbali mapingamizi hayo akisema mahakama hiyo inao uwezo wa kukipokea kwa kuwa uamuzi uliotolewa awali dhidi ya kielelezo hicho, haukumaliza kesi.

“Mahakama inakuwa Funtus Officio ikithibitika kwamba jambo lililopo mbele ya Mahakama limeshazungumzwa na kutolewa maamuzi. Kwamba jambo hilo linatakiwa liwe limeimaliza kesi kwa kumkuta mshitakiwa ana hatia au kuitisha jambo lolote. Amri hiyo ambayo inakuwa imeinyima Mahakama, inatakiwa iwe na matokeo ya kuifikisha kesi mwisho,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga amesema; “ukiangalia kimantiki kielelezo ambacho kimetolewa baada ya kielelezo hicho kukataliwa kilikuwa katika suala la utambuzi, na kwamba upokelewaji wake siyo wa mwisho, basi hata kupokelewa kwake siyo jambo la msingi. Hoja ya Funtus Officio naitupilia mbali kwa sababu nilizoeleza.”

Kuhusu hoja ya kutokuwepo kwa amri ya mahakama ya kukitoa kitabu hicho, Jaji Tiganga amesema haina mashiko kwa kuwa msajili wa mahakama anayo mamlaka kufanya hivyo, kwa mujibu wa Mwongozo wa Utunzaji Kilelezo wa 2020.

“Mahakama hii inaona kwa mujibu wa muongozo wa utunzaji kielezo ya 2020, katika mazingira ya shauri hili iwepo amri ya kukitoa na msajili ana mamlaka ya kukitoa na kwa namna ambavyo nimeeleza naona hoja hiyo pia haina mashiko sababu ya hakukuwa disposal order haina msingi.

“Na hii inapelekea hoja zote tatu zilizotolewa hazina mashiko na hivyo napokea kitabu hicho kama kielelezo namba 2 cha kesi ndogo ndani ya kesi kubwa,” amesema Jaji Tiganga.

Baada ya Jaji Tiganga kutoa uamuzi huo, alielekeza shahidi huyo wa Jamhuri, Ricardo Msemwa aendele kutoa ushahidi wake.

Pingamizi hilo lilitolewa tarehe 17 Novemba 2021 baada ya Askari Mpelelezi, Ricardo Msemwa, wakati akitoa ushahidi wake, kuiomba mahakama hiyo ikipokee kitabu hicho alichodai alikitumia wakati anawaingiza na kuwatoa, mshtakiwa Mohamed Ling’wenya na Adam Kasekwa katika kituo hicho.

Mawakili wa utetezi walidai, kitabu hicho kiliwahi kutolewa uamuzi katika kesi hiyo ndogo wakati shahidi wa kwanza wa jamhuri, Jumanne Mlangahe, alipoiomba mahakama hiyo ikipokee kwa ajili ya utambuzi, ambapo ombi hilo lilikataliwa kwa kuwa hakuweka msingi wa kuaminika kwake na hakukuwa na amri ya mahakama ya kukitoa.

Kutupiliwa mbali kwa pingamizi hilo la utetezi, kunafanya kufikia nane yaliyotupiliwa mbali tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo mwishoni mwa Agosti mwaka huu.

Baadhi ya mapingamizi hayo ni uhalali wa Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, maelezo ya onyo ya mshitakiwa Kasekwa yasipokewe, na hati iliyotumika kufungua kesi hiyo kuwa na makosa ya kisheria.

Mengine; ni hati ya ukamataji mali za washitakiwa Kasekwa na Ling’wenya iliyowasilishwa mahakamani isipokewe na lile lililohusu usahihi wa saini ya shahidi wa nne wa Jamhuri, Anita Mtaro (45), mfanyabiashara wa mbege, Rau Madukani, Moshi, Kilimanjaro.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!