June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mapato ya dhahabu nje ya nchi yashuka

Prof. Benno Ndullu

Spread the love

MAPATO yatokanayo na  mauzo ya dhahabu nje ya nchi, yamepungua na kufikia Dola za Marekani milioni 1,377.2 katika mwaka ulioishia Machi 2015, ikilinganishwa na Dola milioni 2,292.1 mwaka 2012. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Hatua hiyo imechangia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.

Hali hiyo imetokana na kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia na kupungua kwa uzalishaji wa dhahabu nchini.

Akitoa mada kuhusu mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa wabunge mjini Dodoma leo, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof.Benno Ndulu, amesema uzalishaji wa dhahabu katika kipindi hicho ulipungua kutokana na kufungwa kwa baadhi ya migodi nchini ya Tulawaka na Resolute.

Prof.Ndulu amesema bei ya dhahabu katika soko la dunia imekuwa ikipanda na kushuka mpaka kufikia dola za Marekani 1,198.9 kwa aunzi moja kwa mwezi Aprili 2015, ikilinganishwa na kilele cha dola za Marekani 1.771 kwa aunzi ya mwezi Septemba 2011.

“Pia dhahabu iliyouzwa nje ya nchi imepungua kutoka tani 40 kwa mwaka ulioishia  Septemba 2011 hadi kufikia 35.5 kwa mwaka ulioishia Desemba,”amesema.

Aidha, Gavana amesema, mbali na hilo kasi ya kushuka kwa shilingi imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kikubwa kunapokuwapo na matukio yasiyokuwa ya kawaida.

“Kutokana na hali hiyo, BoT imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza viwango vya akiba ambavyo mabenki yanatakiwa kuhifadhi Benki Kuu (SMR) kutoka asilimia 20 mpaka 40 kwa amana za serikali.

“Kupunguza kiwango cha fedha za kigeni ambazo mabenki yanaruhusiwa kubaki nazo, ambazo zinaweza kutumika kutafuta faida kwa miamala ya fedha za kigeni,” amesema Prof. Ndullu.

Kuhusu mwenendo wa thamani ya  shilingi, Prof. Ndulu amesema kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2014, kulingana  na misingi ya kiuchumi imekuwa ikishuka na kupanda ambapo kwa sasa ipo kwa zaidi ya shilingi moja ni sawa dola ya Marekani 1,844.5. 

Prof. Ndulu ameongeza kuwa, ucheleweshaji wa fedha za wahisani na mikopo ya kibiashara kutoka nje ya nchi na kuja kwa uchache kumeathiri soko la fedha za kigeni na kuchochea hisia ya kuwepo kwa upungufu wa fedha za kigeni.

Katika kipindi cha miezi kumi ya kwanza ya mwaka 2014/15, fedha za wahisani zilizopokelewa zilikuwa dola za Marekani milioni 201.9, ikilinganishwa na makisio ya dola za Marekani milioni 542.9.

Pia, serikali ilitarajia kupokea mikopo ya kibiashara kutoka nje yenye thamani ya dola za Marekani milioni 800 lakini hadi Aprili 2015 ni dola za Marekani milioni 310 ndizo zilipatikana.

Gavana Ndulu amesema pamoja na sababu hizo, nyingine ni kama vile msimu wa mapato madogo yatokanayo na utalii wa bidhaa asilia, kuongezeka kwa malipo ya serikali nje ya nchi ambayo yanahusu Tanesco, TRL, mashine za kielekroniki za uandikishaji wapiga kura (BVR).

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuongezeka kwa malipo ya wakandarasi, hisia za upungufu, na wasiwasi kuhusu uchaguzi na sababu nyingine nyingi.

Wakichangia mada hiyo, baadhi ya wabunge walisema ni aibu kwa sekta ya utalii kuingiza kipato kidogo cha Sh. bilioni mbili kwa mwaka licha ya kuwa na vyanzo vingi vya mapato kwa ajili ya kuchochea uchumi.

Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan amesema, BoT imeshindwa kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania. 

Azzan alitolea mfano maduka ya kubadilisha fedha kuwa yapo mengi na yamekuwa yakifanya biashara hiyo bila kutoa risiti jambo ambalo amesema linaikosesha serikali mapato yake halali.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Godluck Ole Medeye amesema ni jambo la ajabu hapa nchini kuruhusu matumizi ya fedha za kigeni huku nchi zingine zinatumia fedha zao kwa kila bidhaa.

Ametolea mfano Malaysia kuwa ni moja ya nchi ambayo inafanya vizuri kutokana na kuwa na msimamo wa matumizi ya fedha yake ya ndani, hivyo kukuza uchumi.

“Unajua mimi sielewi ni kwanini sisi tunaendelea kuruhusu matumizi ya dola na fedha zingine za kigeni kulipia huduma lakini nchi za wenzetu haziruhusu mfano Malaysia,” amehoji Ole Medeye.

Ole Medeye amesema kuonesha kuwa serikali haina nia thabiti ya kuachana na matumizi ya dola hata bajeti yake imeweka viwango vya fedha kwa njia ya dola badala ya kutumia fedha za ndani.

Akijibu hoja hizo, Gavana Ndulu amesema matumizi ya dola yanatumika mara nyingi katika kulipia ada kwa baadhi ya shule na nyumba za biashara na kuongeza kuwa BoT itafuatilia kwa kushirikiana na mamlaka inayohusika ili kuondoa hali hiyo.

Ndulu amesema wawekezaji wanaokuja nchini wanakuja na kadi zao kama watanzania wanavyoenda na kadi zao nje ya nchi na wanapata huduma ya kifedha. 

error: Content is protected !!