July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maoni ya Watanzania juu ya kauli ya Dk. Slaa

Spread the love

BAADA ya kutolewa hotuba ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willbrod Slaa wananchi wa mji wa Dodoma wamepokea hotuba yake kwa mlengo tofauti. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Akitoa maoni yake Askofu Mkuu wa Kanisa la Endtime Haverst (EHC), Dk. Elias Mauza amesema alichokifanya Dk. Slaa ni kuacha kuzungumzia hoja na badala yake amemjadili na kumshambulia mtu mmoja.

“Ni kweli wanasiasa wengi tuko nao makanisani mwetu na kazi yetu ni kuhakikisha tunabadilisha mioyo yao lakini ikumbukwe kuwa wananchi wanahitaji mabadiliko.

“Inapofikia hatua wananchi wanataka mabadiliko hakuna mtu anayeweza kubadilishwa na jambo kubwa zaidi kwa wanasiasa wasikubali kutumiwa ili kuwaaminisha watanzania uongo,” amesema Dk. Mauza.

Kwa upande wao waendesha bodaboda pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo wamesema wanachotaka kwa sasa ni madadiliko ya kiuongozi na kiutawala wala siyo muda wa kuzungumzia mapungufu ya watu wengine.

Mmoja wa waendesha bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Hassani amesema watanzania wamechoshwa kuishi katika maisha ya ukimbizi.

Naye Mzee Juma Hassani amesema CCM ni lazima iendelee kushika madaraka na kitendo cha Dk. Slaa kujiondoa katika siasa ni jambo la ujasiri.

“Tunampongeza zaidi Dk. Slaa kwa ajili ya kuwaonesha wananchi ukweli na kinachofanywa na wapinzani amewafungua macho watanzania ambao wanashabikia wasichokijua,” amesema

Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amewataka watanzania kutokuwa mashabiki wa maandamano ya vyama vya siasa.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na Mwanahalisi Online katika mahojiano maaalum.

Shekhe Rajabu amesema wananchi wanatakiwa kuwa makini kwani Tanzania ya leo ni tofauti na ya juzi au ya miaka kadhaa iliyopita.

Amesema Tanzania ya leo imejaa wasomi tena vijana wadodo wadogo elimu imekuwa katika kila sekta kiuchumi na kiutandawazi, hivyo wanatakiwa kuwa makini na viongozi wanaonadi sera zao.

“Tunaelekea katika uchaguzi hivyo ni vyema tuwe makini na hawa viongozi juu ya sera zao na tuchague nahodha makini atakayeongoza jahazi letu la jamhuri kwa mfano au zaidi ya viongozi waluopita,” amesema Shekhe.

Naye Kiongozi wa kanisa la Gospel Light Ministries International, Mchungaji Julius Nyange aliwashauri watanzania kutokuwa mashabiki na badala yake wawe mstali wa mbele katika kupiga kura kuchangua viongozi bora.

Amesema kumekuwa na tabia ya watu kujitokeza kwa wingi katika maandamano mbalimbali ya vyama vya siasa.

Mchungaji huyo amesema haitakuwa na maana yoyote ile ikiwa watanzania wataishia kufuata misururu ya vyama vya siasa, huku wakishindwa kupiga kura wakati wamejiandikisha katika daftali la mpiga kura.

Aidha amevitaka vyama hivyo vya siasa kuendesha kampeni zake katika kulenga katika kulinda amani na utulivu bila ya kuleta machafuko.

error: Content is protected !!