July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maombi ya kazi sasa kwa mtandao

Afisa Habari wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Kassim Nyaki

Spread the love

SEKRETARIETI ya Ajira katika Utumishi wa Umma, inatarajia kuzindua mfumo mpya wa utumaji na upokeaji maombi ya kazi kwa njia ya mtandao utakaojulikana kama “Recruitment portal”. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Afisa habari wa Sekretarieti hiyo, Kassim Nyaki, amesema lengo la kuanzisha mfumo huo ni kuboresha utendaji kazi wa taasisi katika kufikisha huduma kwa wateja.

Nyaki ametaja lengo lingine kuwa ni kukidhi mahitaji ya wadau, kuwafikia waombaji wengi wa nafasi za kazi na kudhibiti udanganyifu kwa kurahisisha ukaguzi na kuhakiki taarifa za waombaji.

Amesema, mfumo huo utawasaidia waombaji hao kuunganishwa na mifumo ya taasisi mbalimbali, pia kukidhi maelekezo ya sera mbalimbali za utumishi wa umma pamoja na Dira ya Taifa ya mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Nyaki, walifanya majaribio ya kupokea maombi ya kazi kwa kutumia mfumo huo, kwa matangazo ya kazi matano ambayo yaliwahusu waajiri mbalimbali serikalini na kwamba muitikio ulionekana kuwa mzuri wa kupokelewa na watu wengi.

 Amesema, mfumo huo utapunguza changamoto baadhi ikiwemo ya barua kutofika kwa wakati, kupotea kwa kutumia njia ya posta, mrundikano wa barua na kuepuka gharama zisizo za msingi.

“Taratibu za uzinduzi rasmi wa mfumo huu, zitafanyika hivi karibuni, ambapo tunatarajia kupunguza muda wa uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa asilimia 34.

“Tunatoa wito kwa waombaji kazi wote kutumia mfumo huu kwa kuingia katika mtandao wetu http://portal.ajira.go.tz ili kutuma wasifu binafsi (CV) pamoja na vyeti,”amesema Nyaki.

error: Content is protected !!