WAZIRI Kilimo, Japhet Hasunga amewataka Maofisa ugani nchini kuweka mipango kazi yao itakayowawezesha kufanikisha ufanisi wa kilimo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Hasunga ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua mkutano mkuu wa Mwaka wa siku moja wa maofisa ugani wa halmashauri zote nchini uliofanyika jijini Dodoma.
Mkutano huo ambao lengo lake kubwa ni kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kilimo na mifugo ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
Waziri Hasunga alisema kuwa nchi inategemea zaidi maofisa ugani katika kuwezeza mapinduzi ya kilimo na mifugo kwa lengo la kuongeza pato la taifa.
Katika kutekeleza majukumu yao amewataka maofisa ugani kuhakikisha wanawatembelea wakulima na wafugaji kwa lengo la kuwapatia ushauri utakaowawezesha kulima na kufuga kwa njia ya kisasa.
“Inafika hatua unamkuta afisa ugani anamuuliza mkulima kuwa hii ni mbegu gani, yaani baada ya ofisa ugani kumwelekeza mkulima, mkulima anamwelekeza Afisa ugani.
“Tunataka nyinyi maofisa ugani kuwa na takwimu za mashamba ambayo wanayakagua na kutoa maelekezo kwa wakulima kulima kwa kutumia mbegu bora.
“Kama maofisa ugani mtakuwa karibu na wakulima na kuwasaidia vyema ni wazi kuwa kilimo kitaongeza tija na kuwafanya wakulima kulima kilimo cha kisasa zaidi,” alisema Hasunga.
Leave a comment