January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mansour Yusuf Hamid: Nitagombea uwakilishi 2015

Mansour Yusuf Hamid
Spread the love

WIKI iliyopita, tulichapisha hotuba ya Salim Bimani, aliyoitoa kwenye kongamano la Kamati ya Maridhiano Zanzibar inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe nchini, Khassan Nassoro Moyo  lilofanyika kwenye hoteli ya Bwawani. Ni katika kongamano hilo, Mansour Yusuf Hamid, mwakilishi wa Kiembesamaki, Unguja alipopewa nafasi ya kuzungumza kwa mara ya kwanza tangu kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Leo, tunachapisha sehemu ya kwanza ya kilichoelezwa na Mansour kwenye kongamano hilo. Endelea…

Mengi yameshasemwa. Mimi leo sina mengi ya kusema, lakini ninalo la kusema; na nitasema kwa udhati wa moyo wangu, siogopi na sina cha kuogopa…

Mapinduziiiiii (wananchi wanaitikia daimaaaa). Ndiyo maana siogopi mapinduzi, siogopi kwa sababu mapinduzi nayaelewa.

Yale yaliyokuwa sahihi, maana mapinduzi sahihi yanaeleweka, ni freedom (uhuru). Mimi na nyinyi ni watu tulio huru.

Nakuombeni munistahimilie, pengine mliyoyatarajia kuyasikia kutoka kwangu hamtoyasikia, inaweza kuwa hivyo kwamba yale mliyotarajia kuyasikia kutoka kwangu msiyasikie, lakini nakuombeni mliheshimu hilo na mnistahamilie na nikikosea mnisamehe.

Kwa maana, tangu natoka nyumbani kwangu namuomba Mwenyezi Mungu anijalie kauli thabiti; anijalie niwe na kauli ya ukweli; na anijalie nisiwe na kauli za fitna, uchochezi, wala ubaya mwingine.

Hivyo basi, nawaombeni mnistahimilie na pia ikiwa yale mliotarajia hayakuwa, muendelee kuwa wavumilivu.

Ninaanza kwa kuwashukuru sana sana, wananchi wa jimbo la Kiembesamaki. Wamenipa heshima kubwa na imani kubwa  kwa kunichagua kuwa Mwakilishi wao tangu mwaka 2005.

Ninawashukuru sana, sana, sana kwa heshima hiyo. Hilo halikuwa jambo dogo. Lilikuwa jambo kubwa, tena kubwa sana. Ninawashukuru sana na ninawatakia maisha yenye salama, wao na familia zao.

Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwafanyia maisha yao kuwa mepesi na kuwajalia kila la kheri. Naelewa hakuna binadamu aliyekamilika, hivyo basi, ninawaomba kwa unyenyekevu mkubwa, pale nilipowakosea wanisamehe. Mimi katu hawajanikosa, ila ninawashukuru kwa mema waliyonifanyia.

Ninawashukuru pia wote nilioshirikiana nao katika maisha yangu ya kisiasa, ndani ya serikali katika wizara zote nilizozitumikia. Nawashukuru wajumbe wenzangu wa Baraza la Wawakilishi, namshukuru mheshimiwa spika (Pandu Amir Kificho) na watumishi wengine wa baraza kwa namana tulivyoishi kwa wema. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu nao awajalie kila la kheri.

Nimekuwa nikiulizwa maswali mengi sana na waandishi wa habari kila pembe ya dunia, Marekani, Ulaya hadi Uchina; yaani nchi nyingine ndiyo kwanza nimezisikia kipindi hiki. Ilifika hatua mpaka simu inaganda, nimelazimika kutafuta mafundi wairekebishe. Nimeulizwa mengi.

Leo ninataka kujibu baadhi ya yale ambayo nimeulizwa ili yaishe hapa, sioni sababu ya kuendeleza jambo na kwa kuwa mimi sitaki kusemewa, nitasema mwenyewe.

Nimeulizwa na waandishi wa habari yafuatayo: Je, utakwenda mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama wa CCM (Chama Cha Mapinduzi)? Jibu ni kwamba siendi. Sababu ya kutokwenda mahakamani ni mbili za msingi.

Kwanza, mimi nilichaguliwa kwa mapenzi makubwa na heshima kubwa na wananchi wa Kiembesamaki. Sitaki kuwa mwakilishi wa mahakama.

Pili, sina pesa ya kuchezea. Mshahara ndiyo umeshakatika na kwamba sitaki kuendelea na malumbano. Hakuna haja. Waungawana hawalumbani.

Nimeulizwa na waandishi wa habari uchaguzi mdogo nitagombea? Jibu langu, ni hili: Sigombei. Ya nini kuendeleza machungu ya wananchi wa jimbo la Kiembesamaki? Yanini kuendeleza malumbano na siasa za matusi? Hapana. Hakuna haja.

Bali ninawaeleza, ikifika mwaka 2015 na nikiwa hai, nikiwa mzima na bado nikiwa na dhamira na moyo wa kuwatumikia watu, naweza kufikiria vinginevyo.

Nimeulizwa, umechukizwa na kufukuzwa; na kwamba kama nina ugomvi na CCM? Jibu langu ni jepesi sana. Sina ugovi kabisa. Sina. Nitawaambieni kwa nini sina ugomvi.

Ni kwa sababu, hili si jambo dogo. Ni kubwa mno, kwangu mimi  kubwa tena sana na ndiyo maana tulipokuwa tunaimba sisi sote; mimi nililia kwa sababu hili si jambo dogo.

Mimi naitwa Mansour Yusuph Himid, nilitaka mwenyewe kujiunga na Chama Cha Mapinduzi. Sikulazimishwa na mtu yeyote. Kinyume na inavyosemwa, nilikwenda mwenyewe kuitafuta hiyo kadi yangu ya mwanzo mwaka 1987.

Lakini madamu Mwenyezi Mungu amewapa wanadamu midomo waache waseme, ukweli wa nafsi na ukweli wa hali halisi naujua mimi, kwa hiyo mimi sina ugomvi na CCM. Sina.

Nimejenga historia ya undugu na familia ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Kuna wenzangu mle, nimeishi nao kwa hisani kubwa na mapenzi makubwa; mikono ya pole mingi iliyonifika ni kutoka kwa watu wa CCM.

Haya kwangu mimi hayatafutika. Nitaendelea kuwaenzi wenzangu na nitaendelea kuwaheshimu. Maamuzi ya kisiasa ni ya kisiasa, kama nilivyosema sitaki basi.

Wenzangu wamenipima, wameniona sifai kuwa miongoni mwao. Ni haki yao. Ni haki yao kwa sababu, ni chao (chama), ni chao. Mimi simo. Sawa…

Lakini kama nilivyosema, miye mtu huru wala wasidhani, nikiamua kufanya maamuzi yoyote yaliyoko kwenye misingi ya sheria na katiba, nitahofia kuyafanya. Hapana. Nitafanya. Kama kutukana tena hapo haya, kila mmoja atajijua mwenyewe.

Nikaulizwa, utakata rufaa? Ninawajibu, sikati. Yanini, tunarudi palepale, wenzio wameshakupima hawakutaki, namkatia nani tena rufaa? Hapakaliki tena kule, miye siyo mwenzao. Nilimsikia mmoja wao akisema, sisi na yule yameshatuisha. Namimi namwambia, nami yameniisha.

Ninazo hisia zangu kama binadamu, zinaungana na historia yangu na historia ya wazee wangu, lakini sasa si mahala pake wala si wakati wake. Pengine miezi ya mbele, miaka ya mbele, tukiwa tumetulizana, kama nitakuwa nalo la kusema, nitalisema bila wasiwasi. Sitahofia kusema.

Lakini kwa sasa niseme tu kwamba ninawashukuru sana wenzangu, mimi nitaendelea kuenzi historia ya udugu wetu, tena mtashangaa mikoa mingi sana ya bara, viongozi wengi wamenipigia simu, wengine wameshangaa, wengine wakiwa na huzuni kubwa, lakini wote lengo lilikuwa ni kunipa pole na kunitaka nitulizane na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Allahamdulilah nimeshamshukuru Mungu, na ninaendele kumshukuru kwani ndiye wa kutegemewa na liziki kama ipo, itatoka sehemu nyingine. Kama haipo, basi ndiyo mipango ya Mungu. Nikaulizwa na waandishi wengine. Je, upo salama?

Itaendelea wiki ijayo.

error: Content is protected !!