June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mansour Himid kidedea

Spread the love

RUFAA aliyokatiwa Mansour Yussuf Himid, katibu wa mikakati ya ushindi wa Maalim Seif Shariff Hamad, kulenga kumzuia kugombea uwakilishi jimbo la Kiembesamaki, imetupwa. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Uamuzi wa rufaa hiyo umetangazwa na Himid mwenyewe alipopanda jukwaa la uzinduzi wa kampeni ya Maalim Seif kwenye uwanja wa Kibandamaiti, mjini Zanzibar.

Himid amesema watu wasiomtakia mema yeye na Zanzibar wameumbuka kwa sababu uamuzi wa rufaa waliyomkatia wakidai amedanganya taarifa zake kwenye fomu za uteuzi, ni mzuri kwake.

Rufaa hiyo ilikatwa na Mwanaasha Khamis anayegombea uwakilishi jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akisimamiwa na jopo la mawakili walioongozwa na Hamidu Mbwezeleni.

Himid ameahidi kuendelea kusimamia mkakati wa kumpatia ushindi mkubwa Maalim Seif anayegombea urais kwa mara ya tano.

“Nitaendeleza kampeni ya kuwaondolea unyonge kupitia ushindi wa Maalim Seif,” amesema Himid ambaye Agosti 2013, alifukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadaye akatangaza kujiunga na CUF.

“Basi tena kukosa matumaini Wazanzibari, basi tena kuogopa kuona askari, vikosi tulivoundiwa na Serikali ya Mapinduzi ili kusimamisha hishima yetu, leo vinadhalilisha Wazanzibari, vinaua Wazanzibari, vinatumika kukamata masheikh zetu. Halafu viongozi wanasimama hadharani wakitetea yote haya,” amesema.

Amesema, “Tunahitaji kiongozi ambaye atasimamisha utu na hishimaa yetu, umoja wa Wazanzibari, atuunganishe Wazanzibari kwa umoja wetu, tusimamie moja la kwetu Wazanzibari, kila mmoja wetu awe na haki sawa na mwenziwe, kiongozi huyu atakuwa Maalim Seif.”

Himid amesema viongozi wabaya kwa Zanzibar ni wale wanaozungumzia utengano, kufuta umoja, wakiwabagua Wazanzibari.

“Tuzinduke, tuamke, tusikubali kudhalilishwa, tuache woga, tusonge mbele… wache wafanye wanayoyafanya, siku moja tu kufa. Hatuwezi kuendelea kuishi hivi . tutapata kiongozi mzuri ambaye lakini msitarajie atafanya miujiza, tutalazimika kujituma, tutajituma na maendeleo yatatufuata.

Himid aliaga jukwaa akisema, “Wazanzibari mbele kwa mbele tujiamulie, tujitokeze kwa wingi dunia ione, tuache woga, na tufanye maamuzi Oktoba 25.”

Kampeni hiyo pia ilipambwa kwa nasaha za Mzee Hassan Nassor Moyo aliyesema Wazanzibari wote wanaopenda nchi yao wamtilie kura zote Maalim Seif pamoja na wagombea uwakilishi, ubunge na udiwani waliosimamishwa na CUF.

Amesema Maalim Seif ameonesha nia nzuri kwa Wazanzibari tofauti na viongozi wengine ambao “hawataki maelewano, hawataki umoja na hawana uzalendo kwa nchi yao. Hawa wanyimwe kura katika uchaguzi huu.”

error: Content is protected !!