January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mansour anogesha siasa Zanzibar

Mwanasiasa, Mansour Yusuf Himid akisailiama na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, baada ya kukabidhiwa kadi ya uanachama wa chama hicho.

Spread the love

SAFARI ya kihistoria ya mwanasiasa kijana wa Kizanzibari, Mansour Yussuf Himid, ndio kwanza inanoga. Baada ya kutulia akibakia asiye chama tangu alipofukuzwa CCM zaidi ya mwaka sasa, hatimaye amejiunga rasmi na Chama cha Wananchi (CUF), Jabir Idrissa anaachambua zaidi.

Mbele ya halaiki ya wananchi na wanachama wa CUF waliokusanyika mkutano wa hadhara kijiji cha Paje, Wilaya ya Kusini Unguja, mwana huyo wa Mkuu wa Kwanza wa Jeshi la Zanzibar, Yussuf Himid, alichukua kadi ya CUF na kusema ameamua.

Mansour alifukuzwa CCM Agosti 23, 2013 baada ya kuvuliwa uanachama wa chama hicho kwa tuhuma za usaliti dhidi ya sera ya chama kuhusu Muungano wa Serikali Mbili.

Uamuzi wa kumvua uanachama ulikuwa hitimisho la shutuma za muda mrefu ndani ya makada wenzake kwamba amekuwa akijitokeza na msimamo ulio hasi dhidi ya ule wa CCM wa kuamini katika mfumo wa Muungano wa serikali mbili.

Ni uamuzi huo uliochukuliwa baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuongoza kikao cha Kamati Maalum ya NEC, kilichojadili tuhuma dhidi ya Mansour, na kuwezesha kutolewa mapendekezo yaliyopelekwa mbele ya Kamati Kuu.

Kamati Kuu inayokutana chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete ambaye pia ndiye Rais wa Tanzania, iliidhinisha pendekezo la kumvua uanachama Mansour.

Wakati fulani Mansour alisema kilichomponza ni kule kujiamini kwake na kusimama kidete akipigania mamlaka kamili ya Zanzibar dhidi ya unyonyaji inaofanyiwa na Serikali ya Muungano wa Tanzania.

Alikataa kutumia fursa iliyokuwepo kikatiba ndani ya CCM, ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumvua uanachama. Alikuwa na sababu, akisema, “Sina sababu ya kukata rufaa. Nitakuwa nalazimisha kuwa mwanachama wa chama ambacho wenyewe wameshanikataa. Sitakata rufaa wala sitofungua kesi mahakamani. Kama hawanitaki, basi,” alisema.

Kwa msimamo wake wa kuipigania mamlaka kamili ya Zanzibar, chini ya kaulimbiu yake ya “Tuachiwe Tupumue,” Mansour alionekana amechukua msimamo unaosaliti chama chake. Kwamba amekigeuka kwa kuzivaa sera za CUF.

Alibakia Mzanzibari zaidi anayelilia Zanzibar kurejeshewa mamlaka yake kamili, msimamo unaojulikana kushadidiwa na CUF, chama ambacho viongozi wake wamekuwa wawazi wakijitoa mhanga kusimamia kupatikana kwa Muungano wa maridhiano badala ya uliopo kwa miaka yote tangu 1964, unaoonekana kuikandamiza Zanzibar.

Baada ya kushuhudiwa akitoa kauli nzito kupitia jukwaa la makongamano yaliyoandaliwa na Kamati ya Maridhiano ambayo alikuwa mmoja wa wajumbe wake, ikiongozwa na muasisi wa mapinduzi, Mze Hassan Nassor Moyo, Mansour alianza kuhutubia mikutano ya CUF, kwa muda mfupi kama kusalimia tu wananchi.

Ikawa hakosi kuhudhuria mikutano ya CUF hasa iliyohutubiwa na Katibu Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye Agosti mwaka huu, baada ya Mansour kutungiwa kesi ya kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria, alisema kadhia hiyo ni ishara njema kuwa mambo mazuri yanakuja.

Baada ya kukaa ndani kwa siku kadhaa, Mansour, ambaye alipekuliwa nyumbani kwake Chukwani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, alipata dhamana na kuwa nje. Mpaka sasa kesi haijaanza kusikilizwa.

Anajiunga na CUF wakati tayari alishapewa jukumu la kuongoza kiitwacho Kamati ya Mikakati ya kumpeleka Maalim Seif Ikulu kwa uchaguzi mkuu wa 2015, huku akiahidi kuwa kura yake itakuwa ya kwanza kwa kiongozi huyo na kwamba atapigania kuzipata kura nyingi uchaguzi utakapofika.

“Ninatoa ahadi hii kwa sababu ninaamini Maalim Seif ndiye unayefaa hasa kuwa Rais wa Zanzibar. Wazanzibari wanaimani sana nawe na wanakutarajia uwaongoze. Ndio maana nimejitolea kuhakikisha unapata kura nyingi katika uchaguzi ujao,” alisema.

Bila ya shaka msimamo wake huo umeongeza uchangamfu wa siasa Zanzibar, kwa kuwa ameshaahidi kuwa ataligombania jimbo la Kiembesamaki kwa chama atakachojiunga. Kujiunga CUF kunathibitisha sasa kuwa Mansour atagombea uwakilishi kwa tiketi ya chama hicho.

  • Alizaliwa tarehe 3 Novemba 1967 mjini Unguja. Alisomea elimu ya msingi na sekondari nchini India kati ya mwaka 1976 na 1987. Alizivaa rasmi siasa mwaka 2000 alipoteuliwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati huo akiwa maarufu miongoni mwa vijana wa Mji Mkongwe ambako akifanyia shughuli zake za biashara ya hoteli.
  • Aligombea uwakilishi jimbo la Kiembesamaki katika uchaguzi wa 2005 kupitia CCM, chama ambacho familia yake ikikiamini na kukipigania. Alichaguliwa kwa asilimia 94 ya kura zote.
  • Aliingia katika safu ya uongozi wa juu wa chama tangu 2002. Aliteuliwa Mweka Hazina wa Chama chini ya Sekretarieti ya Zanzibar iliyoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Saleh Ramadhani Ferouz. Aliondolewa mwaka 2012 katika kile kilichoitwa aliomba kupumzishwa shughuli za chama.
  • Serikalini alianza kwa kuteuliwa Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Ardhi na Mazingira. Na akapandishwa kuwa Waziri wa wizara hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa 2005. Ilipoundwa serikali baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, Mansour alihamishiwa Wizara ya Kilimo na Maliasili.
  • Pia amekuwa Mjumbe katika Baraza la Biashara la Zanzibar tangu 2002 hadi 2012.

Wajumbe wenzake katika Kamati ya Maridhiano iliyofanikisha mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, ni Mohamed (Eddi) Riyami waliokuwa CCM, pamoja na Ismail Jussa Ladhu, Salim Bimani na Abubakar Khamis Bakary kutoka CUF.

error: Content is protected !!