December 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maneno ya mwisho ya Maalim Seif kwa Zitto

Spread the love

 

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema, wosia wa mwisho aliopewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ni kuhakikisha chama chake kinaimarisha maridhiano visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Zitto amesema wosia huo leo Alhamisi tarehe 18 Februari 2021, katika maziko ya mwili wa Maalim Seif, yaliyofanyika kijiji cha kwao, Nyali, Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar.

Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, kupitia ACT-Wazalendo, alifariki dunia Jumatano ya tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu tangu 9 Februari 2021.

Akitoa salamu za ACT-Wazalendo, Zitto amesema, Maalim Seif, alimuachia wosia huo akiwa ofisi kwake mjini Unguja, siku moja kabla hajapata tatizo lililosababisha kifo chake.

“Siku moja kabla ya kukutwa na tatizo liliosababisha umauti wake, nilizungumza nae ofisini ya makamo wa kwanza wa rais pamoja na mambo mengine, alinistisitiza sana kuhakiksiha kwa vyovyote iwavyo, chama chetu kinakuwa mstari wa mbele kuimarisha maridhiano,” amesema Zitto.

Zitto amesema “ sikujua kumbe alikuwa ananiaga, nafahamu kuwa siku hiyo alikutana pia na mawaziri wako wawili Rais (Dk.Hussein Mwinyi), sijui wenzangu wosia wao ulikuwa nini.”

Maalim Seif alianza kuumwa tarehe 29 Januari 2021, ambapo alilazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Zanzibar, hadi alipohamishiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyoko kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

Zitto amesema, ACT-Wazalendo kitauenzi wosia huo, pamoja na fikra za Maalim Seif (77), katika kuhakikisha Zanzibar inakuwa na umoja.

“Kwa hakika mwisho wa Maalim Seif duniani sio mwisho wa mawazo na fikra zake, bali ni mwanzo wa kutekeleza maono yake kwa aina ya Zanzibar aliyopenda kuijenga pamoja na Wazanzibar wote,” amesema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo amesema, chama hicho kitaendelea kumpa ushirikiano Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, katika kuiendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

“Sisi ACT-Wazalendo, tutaendelea kutoa mchango wetu kwa serikali ya umoja wa kitaifa ili kuhakikisha ndoto za Maalim Seif kuleta ustawi, haki na umoja kwa Wazanzibar inakamilika,” amesema Zitto.

Serikali hiyo iliundwa kufuatiwa maridhiano baina ya Maalim Seif na Rais Mwinyi, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kumalizika.

Katika uchaguzi huo, Rais Mwinyi alitangazwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar na Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC), huku Maalim Seif aliyekuwa mpinzani wake wa karibu kupitia ACT-Wazalendo, akishika nafasi ya pili.

Akielezea maridhiano ya marehemu Maalim Seif na Rais Mwinyi, Zitto amesema, ACT-Wazalendo kitaendelea kumuamini kiongozi huyo wa Zanzibar, kama alivyokuwa anaaminiwa na Maalim Seif.

“Rais Mwinyi, Maalim Seif alikuamini sana, alikupa moyo wake wote na alikuwa akituambia namuamini Dk. Mwinyi. Na alikuwa anarudia kwa wale tuliokuwa na mashaka na maridhiano, alikuwa anahimiza kwa neno hilo nina imani na Dk. Mwinyi,” amesema Zitto.

Zitto amewahakikishia Wazanzibar kwamba, ACT-Wazalendo kitaendeleza harakati zilizoasisiwa na Maalim Seif, katika kuhakikisha visiwa hivyo vinakuwa na maridhiano.

error: Content is protected !!