July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Manara: Tukifungwa na Yanga Kigoma naacha kazi

Haji Manara

Spread the love

 

KUFUATIA klabu yake ya Simba kupoteza mchezo wao dhidi ya Yanga, kwa bao 1-0, Afisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara ameahidi kuwa kama wakifungwa tena na watani wao kwenye mchezo wa Fainali Kigoma, ataacha kazi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Simba ilipoteza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa bao 1-0, lilifungwa na Zawadi Mauya dakika ya 11 kipindi cha kwanza, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi iliyopita tarehe 3 Julai, 2021.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, msemaji huyo aliwataka wachezaji wa klabu ya Simba kujua thamani ya nembo ya klabu hiyo mara baada ya kuwaangusha kwenye mchezo huo.

“Nahodha John Bocco, sema na wenzio kaka, mtakuja kuua watu kwa makundi siku moja, naambiwa Dar kuna shabiki kajipiga kitanzi huko, kipindi cha kwanza mmecheza kama mmelazimishwa au mnadai kitu, mmezinduka kipindi cha pili na wao wakaweka kontena mechi ikaisha.”

“Wallah Kigoma tukifungwa naacha hii kazi narudi shamba kulima, viongozi wanatimiza majukumu yao, washabiki wanajaa kuliko washabiki wao kwa mbali mno, mimi natukanwa kutwa kwa kuwapa nguvu nyie lakini mmeenda kutuangusha,” Aliandika Manara.

Simba itakutana tena na Yanga, kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), tarehe 25 Julai, Mkoani Kigoma.

Aidha Manara aliendelea kuandika kuwa, wachezaji wa klabu ya Yanga, walijitoa kwa asilimia kubwa, ukilinganisha na wachezaji wa Simba.

“Sioni sababu ya kuendelea na kazi hii kama wachezaji hawajui nini maana ya uzito wa mchezo wa Simba na Yanga. Wachezaji wao wanajitoa asilimia elfu moja toka dakika ya kwanza, sisi tunazinduka kushakuchwa, kaeni wenyewe zungumzeni na thamani ya jezi ya Simba ilindwe.”

error: Content is protected !!