Monday , 11 December 2023
Home Kitengo Michezo Man United: Duniani hakukaliki, Akhera hakuendeki
Michezo

Man United: Duniani hakukaliki, Akhera hakuendeki

Spread the love

MCHEZO wa leo saa 4:00 usiku wa Ligi Kuu ya England kati ya Manchester United na Manchester City (Manchester Debby) kwenye uwanja wa Old Trafford, unawaweka njia panda mashabiki wa United. Anaandika Yusuf Aboud (Babu Jongo) … (endelea).

Niseme mapema tu kwa wale wasionijua, kwamba mimi ni mshabiki wa Liverpool, ingawa sio miongoni mwa wale wa kulialia.

Kwa upande mmoja mashabiki wa United wanatamani timu yao iifunge City, hasa kwa kuzingatia katika kipindi hiki cha takriban miaka kumi tangu City inunuliwe na Sheikh Mansour, United haina uhakika wa kuifunga City, lakini pia United haijafuta kidonda cha kukandikwa 6-1 na City. 

Kwa upande wa pili, mashabiki haohao wanatamani timu yao ifungwe na City, lengo likiwa kuiharibia Liverpool isinyakue ubingwa wa England msimu huu. Ikumbukwe mahasimu wa soka la England ni Liverpool na Manchester United, ingawa City na United wana ule uhasama wa kutoka mji mmoja wa Manchster – yaani Manchester Debby.

Kwa United ni afadhali wafungwe na City kuliko kuirahisishia ubingwa Liverpool. Mpaka sasa United inaongoza kubeba ubingwa wa England mara 20 ikifuatiwa na Liver iliobeba mara 18, lakini kabla ya mwaka 1990, Liver ilikuwa tayari imeshanyakuwa mara hizo 18 na United ilinyakuwa mara 7 tu. Ndiokusema Liverpool ina njaa ya ubingwa kwa takriban miaka 30 sasa.

Kabla ya mchezo wa leo usiku, Liverpool inaongoza Ligi ikiwa na point 88, ikifuatiwa na City yenye point 86, lakini Liver imecheza michezo 35 na kubakisha michezo mitatu, huku City imecheza 34 na kubakisha minne.

Bahati mbaya kwa United mcheo wa leo unafaida na hasara kwao, ikikubali kufungwa kwa upande mmoja itakuwa imeiwekea ngumu Liver kutwaa ubingwa, sababu City itarudi kileleni mwa Ligi ikiwa na point 89 na michezo mitatu mkononi, lakini kwa upande mwingine United itakuwa imejihakikishia kujiondoa kwenye mbio za kuwania Top Four, nafasi itakayoiwezesha kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Kisa hiki cha leo kwa mashabiki wa United, kinanikumbusha hadithi moja aliyonisimulia bibi yangu enzi za uhai wake; Sharifa Bint Athuman Bin Jumaa, almaarufu Bi. Gari.

Bi. Gari alinihadithia kuwa; siku moja Mfalme akaita raia wake wote, akawapanga kwenye mstari na kuwaambia kila mmoja ataje kitu anachokitaka au jambo analolitaka afanyiwe na Mfalme, naye bila kusita atatekeleza.

Mmoja miongoni mwa raia wake (tuiite United) alikuwa na wivu kwa rafiki yake, hakupenda kuzidiwa chochote na rafiki yake huyo. Akapanga kukaa nyuma yake kwenye mstari, ili atakachokitaka kwa Mfalme yeye aseme mara mbili yake.

Bahati mbaya rafiki yake (tuiite Liver) alishajua alichokipanga mwenzake aliyekaa nyuma yake, naye kwa roho mbaya akataka kumkomoa. Ilipofika zamu yake kusema anachokitaka kwa Mfalme, wakati anajiandaa kusema yule rafiki yake wa nyuma akarukia hata kabla mwenzake hajasema, “…mimi utanipa mara mbili ya utakachompa rafiki yangu.”

Yule jamaa wa mbele alivyoona rafiki yake karopoka, akamwambia Mfalme, “Mfalme nataka unitoe jicho moja niwe chongo,” akageuka nyuma akamwangalia rafiki yake akacheka. Maana yake rafiki yake atatolewa macho mawili ili awe kipofu.

Manchester United ikifungwa leo maana yake itakosa kuingia kwenye Top Four lakini pia haiwezi kujihakikishia kuikosesha ubingwa Liverpool. Sababu kuna mechi nyingine tatu ambazo City ili abebe ubingwa italazimika kushinda zote.

Hata hivyo, United ya sasa ni dhaifu, haina uthubutu wa kuifunga City hata kama itaamua kukaza, hivyo basi mashabiki wa United wasubiri tu kudra za Mungu. Wakubali majaaliwa yao. Upofu unawakaribia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Michezo

Vijana waadhimisha miaka 62 ya Uhuru kwa kushiriki michezo

Spread the loveUMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) tawi la Mlowo, jana...

Michezo

Pesa ipo huku Meridianbet, beti sasa

Spread the love  WIKIENDI inaishia leo hii jaman kama bado hujasuka mkeka...

Michezo

Wenzako wameshakuwa mamilionea hapa wewe unasubiri nini?

Spread the love  WIKIENDI imefika na ukiachana na mvua za Dar es...

Michezo

Manchester City vichwa chini Ligi Kuu England

Spread the love MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Uingereza klabu yaManchester City...

error: Content is protected !!