May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Man U kwawaka moto, Martial amvaa kocha mpya

Spread the love

 

Mshambuliaji wa mashetani wekundu, Anthony Martial amekanusha madai kuwa alikataa kujumuishwa kwenye kikosi cha Manchester United kilichocheza dhidi ya Aston Villa. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea)

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Uingereza, iliyopigwa siku ya Jumamosi tarehe 15 Januari, 2022, Manchester United ambao walikuwa wageni wa Aston Villa, walilazimishiwa sare ya 2-2 hali iliyozidisha mwenendo mbaya wa timu hiyo.

Akielezea sababu za Martial kukosekana kwenye kikosi chake, Kocha wa muda wa Manchester United, Ralf Rangnick alisema Martial raia wa ufaransa alikataa kujumuishwa kwenye kikosi.

Hata hivyo, Anthony Martial amejitokeza na kukana madai ya kocha Ralf akisema hajawahi kukataa kuchezea klabu hiyo.

“Sijawahi kamwe kukataa kuichezea Man Utd. Nimekuwa hapa kwa miaka saba na sikuwahi kudharau na sitawahi kudharau klabu na mashabiki,” alisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26.

Bila huduma za Martial, Man United walishindwa kupata ushindi dhidi ya Aston Villa mechi hiyo ikitamatika kwa droo ya 2-2.

United walipoteza nafasi ya kuiondoa Tottenham Hotspur kwenye nafasi ya sita na sasa wanashikilia nafasi ya saba wakiwa na alama 32.

Malumbano hayo ndani ya Old Trafford, yamekujia baada ya Martial (26), kumwelezea Rangnick awali kwamba angelipenda kuondoka klabuni hapo mwezi huu.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Mashetani Wekundu mwaka 2015 akitokea AS Monaco na sasa anahusishwa pakubwa na kutokomea Sevilla.

Martial hajachezeshwa katika mechi yoyote ya EPL tangu Oktoba 2021, na pia hajajumuishwa kwa michezo yoyote ya United tangu Disemba 2021.

Nguli huyo amewafungia miamba hao wa Uingereza mabao 50 katika michezo 173 ya EPL.

Januari 2019, chini ya Ole Gunnar Solskjaer, fowadi huyo alitia saini mkataba mpya ambao utaendelea kufanya asalie katika klabu hiyo hadi mwaka 2024.

error: Content is protected !!