MWITIKIO wa wanachama na Watanzania wanaojitokeza kuchangia gharama za mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, umezidi kuongezeka ambapo hadi sasa zimekusanywa fedha kiasi cha 9.9 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetyu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yamesemwa leo tarehe 20 Januari 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala Kanda ya Pwani, Patrick Assenga, akizungumza na MwanaHALISI Online, kuhusu zoezi la michango hiyo inayoendelea kukusanywa na Chadema.
Assenga amesema fedha hizo ni kati ya kiasi Sh. 15 milioni, ambazo ni bajeti iliyopangwa kugharamia mapokezi ya Lissu na mikutano miwili ya hadhara.
Amesema michango hiyo inatoka kwa wanachama wa Chadema na wananchi wa kawaida, ambapo zoezi hilo litafungwa baada ya fedha zilizopangwa katika bajeti hiyo kukamilika.
Katika hatua nyingine, Assenga amesema maandalizi ya kumpokea Lissu yamefikia asilimia 90, hivyo wananchi wajiandae kumpokea tarehe 25 Januari mwaka huu, atakapowasili nchini akitokea Ubelgiji, alikokwenda Novemba 2020, baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu.

“Tunakwenda vizuri Watanzania wanahamasika na ujio wa Rais wa mioyo ya Watanzania kwa hiyo mambo yanaenda vizuri na maandalizi yamekamilika kwa asilimia 90, tumebakia na masuala ya kufunga vyombo vya muziki uwanjani katika Viwanja vya Buriaga Temeke,”
“Taratibu zote zimekamilika Polisi tayari wamepitisha na wameahidi watatoa ushirikiano wa kutosha, hivyo imebaki Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza,” amesema Assenga.
Akitaja baadhi ya matumizi ya fedha hizo, Assenga amesema kutakuwa na vikundi vya ushereheshaji maarufu kama kigoma cha Uruguay, mchango wa mafuta kwa ajili ya pikipiki zitakazobeba wanachama wanaokwenda kumpokea Lissu kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Matumizi mengine ni maandalizi ya uwanja ambao Lissu atakwenda kuzungumza na wananchi, baada ya kurejea.
Hapo sawa.