July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mameya Ilala, K’ndoni kuchaguliwa kesho

Spread the love

BAADA ya uchaguzi wa Mameya wa Halmashauri mbili za Ilala na Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuahirishwa katika mazingira yaliyojaa utata, sasa madiwani wa Ilala na Kinondoni wametangaziwa uchaguzi kufanyika kesho Januari 16. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Awali, uchaguzi huo ulitakiwa kufanyika Januari 9 mwaka huu, lakini ulizuiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatia kesi iliyotajwa kufunguliwa na kada wa CCM aitwae Elias Nawela akiomba mahakama itoe zuio la uchaguzi.

Shauri la Nawela lilisikilizwa juzi na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Respicius Mwijage akaondoa zuio ikiwa na maana kuruhusu uchaguzi huo kufanyika.

Hakimu Mwijage alisema mlalamikaji aliishangaza mahakama kwa kushindwa kuwasilisha hati ya madai ili kukidhi matakwa ya kisheria na kujenga uhalali wa uharaka wa kesi hiyo kama alivyoomba.

“Mlalamikaji alikuwa anajua uhalali wa kesi yake na hajaonyesha sababu yoyote ya msingi iliyomfanya kushindwa kuwasilisha hati ya madai kwa upande wa mlalamikiwa hadi leo hii (Jumatano) kesi ilipokuja hapa kwa ajili ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Mwijage.

Hatua hiyo imekuja wakati upande wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walikimbilia mahakamani nao kuomba kuunganishwa katika kesi aliyoifungua Nawela.

Uchaguzi uliahirishwa siku ambayo maandalizi yalikuwa tayari kuwezesha uchaguzi kufanyika. Ghafla Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala na pia wa Kinondoni walisoma zuio la mahakama kutaka uchaguzi usifanyike.

Uamuzi huo ulizusha mtafaruku kwa kuwa ilionekana ni mbinu ya CCM kutaka kujipanga upya baada ya kuona mpango wake wa kuongeza mamluki wa kupiga kura kama madiwani, kushindikana.

CCM iliingiza mamluki siku ya kwanza ya uchaguzi, wakazuiwa na uchaguzi ukashindikana. Januari 9 ikawa siku nyingine uchaguzi ndio ukaingia kikwazo kwa kuwa hata UKAWA nao waliingiza mamluki.

“Hakuna kesi ya maana mahakamani. Hizi ni mbinu tu za CCM kutaka kuvuruga ili washinde umeya. Leo wameona tumewazidi idadi ya madiwani kwa kuwa nasisi tumeleta madiwani wa viti maalum kutoka Pemba. Tupo mbele kuliko wao,” alisema mmoja wa madiwani wa Ukawa jijini Dar es Salaam.

Kuahirishwa kwa uchaguzi kwa sababu ya zuio la mahakama, kulimsukuma Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki kuhakikisha uchaguzi uwe umefanyika ifikapo Januari 16, mwaka huu.

Jana baada ya kufahamika kwamba mahakama imeondoa zuio la uchaguzi, viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walisema watashiriki uchaguzi na wamejipanga kushinda kwa kuwa wana madiwani wa kutosha kuliko CCM.

Walisema uchaguzi utawezekana iwapo Mkurugenzi wa Halmashauri atafuata sheria ikiwemo agizo la Waziri Simbachawene kwamba kisheria, madiwani wanaopaswa kushiriki uchaguzi huo ni wale ambao wakati wa uchaguzi mkuu, vyama vyao viliwapitisha kugombea maeneo wanayoshiriki kuchagua mameya.

error: Content is protected !!