July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mambo yetu kama Pwagu

Spread the love

MIAKA ile ya 1970 hadi 1980 kilikuwepo kipindi cha Pwagu na Pwaguzi, kila siku za Jumatano majira ya saa 11.00 hivi jioni.

Hawa jamaa walikuwa mabingwa wa kuanzisha kampuni na kubuni miradi. Waliweka matangazo makubwa, na ingawa hawakuwa na vifaa na weledi, waliomba kazi hata zilizowazidi uwezo.

Siku moja walianzisha kampuni ya kuua viroboto, mende, kunguni na wadudu wote watambaao na warukao.

Kazi ikapatikana. Wakaifanya kwa kutumia fimbo na virungu. Wee! Walivunja vikombe, sahani; walizua balaa kubwa. Acha bwana!

Pwagu na Pwaguzi hawapo, wametangulia mbele ya haki, lakini huku nyuma kuna viongozi tena wakubwa wa nchi hii walioiga akili na stadi yao ya kuanzisha mradi wa kupambana na mchwa atafunaye fedha katika halmashauri. Vifaa vyao vya kazi ni maneno.

Hawa jamaa, hawa wakubwa walitamba wakati wa uzinduzi wa Bunge mwaka 2005 kwamba mchwa wote wanaotafuna fedha za halmashauri watauawa kwa Dudu Killer. Mchwa hao walitulia na walipoona hakuna kishindo cha kuchimbua vichuguu ili wawamwagie dawa, waliendelea kutafuna kwa raha.

Mchwa wana akili; walituma askari wa upelelezi kujua kama nzige waliovamia Benki Kuu na kutafuna majani ya EPA wamekamatwa. Askari wakarejesha majibu kwamba wamesamehewa.

Mchwa wakatuma askari wengine kupeleleza kama waliotafuna kupitia kampuni za Meremeta, Richmond, Rada, IPTL wamekamatwa. Askari wakarejesha majibu kwamba wala hakuna mpango.

Mchwa wakavimba kichwa; wakatafuna na kutafuna baadaye wakagundua kwamba njia pekee na salama, ya wao kutobughudhiwa ni kuwa na kadi ya kijani ya Chukua Chako Mapema.

Wakagundua, tena kwa ushahidi, kwamba hata Mkurugenzi Asiyeshitaki (DnPP) hahangaiki na mashitaka ya makada wa kadi ya kijani.

Unabisha? Wale waliokuwa viongozi wizara isiyo-siha na ile wizara ya kusambaza giza nchini, tangu Aprili mwaka jana uchunguzi wao bado haujakamilika.

Yule aliyenaswa na silaha feki dhidi ya Ukimwi, DnPP anasema mashtaka magumu. Aliwahi kutupilia mbali  uchunguzi wa rushwa dhidi ya mkuu wa wizara aliyekukuruka usiku na mkataba kuusainia London.

Mchwa wakashangilia. Hatua zilizochukuliwa dhidi ya mchwa wa Bwagamoyo na Sumuyu waliona ni kumwagiwa jivu. Jivu lieu mchwa?

Sasa turudi katika uhalisia.

CCM haiui mchwa ila inafurahia. Si umeona kule Bukoba, CCM wachache waliookoka walipounga mkono meya atimuliwe kwa tuhuma za kuanzisha kilichodaiwa kuwa miradi ya kifisadi, Babu na Bibi wamekuja juu.

Wanasema kuwa kwani chakula cha mchwa si pambana na hela zilizokaa kihasara? Kwanza hao madiwani wamepewa dawa na nani ya kuua hao mchwa?

Meya asiondolewe wala madiwani wasiondolewe, wote wabaki. Kuleni nchi.

Kwa hiyo hata habari kwamba kuna vigogo 70; eti wakurugenzi wa halmashauri za wilaya wamekula fedha, kwa CCM ni uchuro. Si wanachukua chao mapema? Kuna kosa gani?

Kwamba, madiwani pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero wanamsuta mkurugenzi kwa kufisidi fedha za halmashauri; ni uchuro kwa serikali ya CCM.

Matangazo makuuuuuuuuuuubwa kwamba mchwa wanaotafuna fedha za halmashauri watamwagiwa Dudu Killer; lakini huyo anayetangaza hivyo hana dawa  wala ujuzi. Ni kama Pwagu na Pwaguzi.

Kule barabara miezi mitatu tu, lami kwao; majengo ya shule yanaanguka; baadhi ya miradi  haipo lakini fedha zimeliwa. Zawadi nzuri wanayopewa jamaa hawa – mchwa – ni kuhamishwa. Umeharibu hapa. Nenda paleee!

error: Content is protected !!