August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mambo yatakayotumika kuwapima Wakurugenzi, wakuu wa Idara

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Spread the love

 

SERIKALI nchini Tanzania imesema inakusudia kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu hususan usimamizi wa mapato na makusanyo ya ndani pamoja na upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma …  (endelea).

Watendaji hao pia watapimwa kwa namna wanavyosimamia mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Alhamisi, Tarehe 30 Juni, 2022 wakati akitoa Hoja ya Kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma.
Amesema hatua hiyo ni katika kuhakikisha dhamira nzuri ya Rais Samia Suluhu Hassan inayojiakisi kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 inafikiwa.

Majaliwa amesema Serikali imejipanga vema kuendelea kusimamia suala la uwajibikaji katika utumishi wa umma kwa kuweka mikakati mbalimbali. “Mikakati ipo katika kuimarisha uwajibikaji hususan kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni pamoja na kupima utendaji wa utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara.”

Amesema mkakati mwingine ni kongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka Sh57. 44 bilioni hadi Sh79. 09 bilioni ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hizo.

“Sambamba na ongezeko hilo la Bajeti katika mwaka 2022/2023, Serikali pia, imehuisha muundo wa Sekretarieti za Mikoa kwa kuboresha iliyokuwa Sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa Sehemu ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ili kuimarisha ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.”

Amesema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Madiwani, Mafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kupitia Programu ya Uimarishaji Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuongeza uelewa wa majukumu yao kisheria, kuimarisha mahusiano yao na viongozi wa kisiasa na kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kujenga mifumo na miundo wezeshi katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo. “Eneo hili linahitaji uwepo wa mifumo na miundo imara ambayo itawezesha kujenga msingi thabiti wa usimamizi wa utendaji kazi wa Serikali.”

Amesema hatua hizo zinajumuisha kupitia upya miundo na majukumu ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuziimarisha pamoja na kujenga uwezo wa watumishi katika eneo hilo.

error: Content is protected !!