October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mambo matatu yajirudia kesi ya Mbowe, wenzake

Spread the love

 

MAMBO matatu yamejirudia kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021, inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano, Mkoa wa Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Mambo hayo yamejirudia katika kesi ndogo na kesi ya msingi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka sita ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, wakati mashahidi wawili wa Jamhuri, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Ramadhan Kingai na aliyekuwa msaidizi wa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Arusha, Mahita Omari Mahita, wanatoa ushahidi wao mahakamani hapo.

Jambo la kwanza lililojirudia leo Ijumaa, tarehe 17 Septemba 2021, mahakamani hapo mbele ya Jaji Mustapha Siyani, ni la washtakiwa wawili katika kesi hiyo, kuhamishiwa Kituo cha Polisi Mbweni, wakitokea Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Ambapo Mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Dickson Matata, katika nyakati tofauti walimhoj Mahita sababu za washtakiwa hao wawili kuhamishiwa Mbweni badala ya Kituo Kikuu cha Polisi.

Akijibu swali hilo, Mahita alidai watuhumiwa wawili, Kasekwa na Ling’wenya walipelekwa Kituo cha Polisi Mbweni, kwa sababu ya usalama kutokana na washtakiwa hao kuwa na mafunzo ya ukomandoo kutoma Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Pia, Mahita alidai, watuhumiwa hao walipelekwa kituoni hapo kwa kuwa kulikuwa na nafasi ya kuwatenganisha kila mmoja peke yake, kwa ajili ya kuzuia upelelezi usiharibike.

Mara ya kwanza suala hilo lilibuka wakati Kamanda Kingai anahojiwa na mawakili wa utetezi mahakamani hapo, ambapo aliuliza kama washtakiwa waliwahi kufikishwa katika kituo hicho.

Nashon Nkungu, wakili wa utetezi akimhoji Mahita, imekuwaje wamewapeleka Mbweni wakati kituo kikuu cha polisi ni kikubwa kwa maana kina ofisi ya RPC, Ilala, ZCO, Kamanda wa Kanda Maalum, Mahita alisema ni kutokana na aina ya watuhumiwa wenyewe.

Jambo jingine lililojirudia mahakamani hapo, ni sababu za washtakiwa hao wawili kutofikishwa mahakamani kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya, ambapo Mahita ambaye ni mtoto wa aliyewahi kuwa IGP Omary Mahita alidai inawezekana kosa hilo likawa na uhusiano na kosa la kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, ambalo washtakiwa wameshtakiwa nalo.

Swali hilo pia aliulizwa Kamanda Kingai wakati anatoa ushahidi wake, katika shauri dogo la kesi hiyo mahakamani hapo, ambapo yeye alijibu akidai kosa hilo linaingia katika kesi ya jinai ambayo haifi.

Jambo la tatu, lililojirudia, ni iwapo notebook iliyotumika na askari polisi kurekodi maelezo ya watuhumiwa wakati wanakamatwa mkoani Kilimanjaro, iliwasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo wakati wa ushahidi.

Akijibu swali la Wakili Kibatala, Mahita alidai kifaa hicho ni cha polisi kwa ajili ya kuhifadhia kumbukumbu.

Swali hilo pia aliulizwa Kamanda Kingai juzi, akihojiwa na mawakili wa Jamhuri, ambaye alijibu akidai sio lazima kuileta mahakamani notebook akidai ni kifaa muhimu cha askari polisi ambapo kila kinachoandikwa ni siri kwa ajili ya kujikumbusha.

Mashahidi hao wa Jamhuri, Kamanda Kingai, ambaye alikuwa Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Arusha na Inspekta Mahita, wametoa ushahidi wao mahakamani hapo, katika shauri dogo la kesi hiyo.

Shauri hilo lilitokana na mapinganizi ya mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, wakipinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama kielelezo na Kamanda Kingai, katika kesi ya msingi, wakidai yalichukuliwa nje ya muda kisheria.

Pia, katika mapingamizi hayo walihoji kwa nini mtuhumiwa alihojiwa Dar es Salaam, badala ya Moshi mkoani Kilimanjaro alikokamatwa.

Jaji Siyani aliahirisha usikilizwa wa shauri hilo dogo hadi Jumatatu, tarehe 20 Septemba 2021, ambapo Mahita ataendelea kutoa ushahidi wake. Jamhuri imepanga kutumia mashahidi saba katika shauri hilo dogo.

error: Content is protected !!