Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mambo matatu mazito kwenye kesi ya Lissu
Habari za SiasaTangulizi

Mambo matatu mazito kwenye kesi ya Lissu

Spread the love

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amemnyima aliyekuwa mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, maamuzi ya kumvua ubunge wake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Aidha, Spika Ndugai amegoma kumpa Lissu nakala ya barua aliyomuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, akimjulisha kuwa jimbo la Singida Mashariki, mkoani Singida, limekuwa wazi kufuatia aliyekuwa mbunge wake, kukosa sifa ya kuendelea kuwa mbunge.

Vilevile, mbali na kunyimwa maamuzi ya kuvuliwa ubunge na Spika na kunyimwa barua iliyokwenda kwa mwenyekiti wa NEC, Lissu ameshindwa kupata nakala ya gazeti rasmi la serikali (GN), kutoka kwa mpigachapa mkuu wa serikali, linaloeleza kuwa jimbo lake la uchaguzi, liko wazi.

“Ni vigumu kuamini, lakini ndio hivyo. Spika amefanya maamuzi yake, lakini anagoma kutoa maamuzi hayo kwa aliyefaathirika ili aweze kuchukua hatua. Hili ni jambo ambalo linaweza kufanyika Tanzania pekee,” ameeleza kaka mkubwa wa Lissu, aitwaye Alute Mughwai.

Anasema, “mpaka tunafungua shauri mahakamani, Spika Ndugai, hakutupa barua ya kumvua ubunge Lissu. Hakutoa barua aliyomuandikia mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na hatukuweza kupata nakala ya GN (gazeti la serikali), lililochapishwa likieleza kuwa jimbo la Singida Mashariki, liko wazi kama ambavyo sheria zinavyoelekeza.”

Lissu kupitia kwa kaka yake huyo, amefungua shauri Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Spika Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kupinga kuvuliwa ubunge. Kesi yake imesajiliwa mahakamani hapo na kwa Na. 18 /2019.

Spika Ndugai aliutangazia ulimwengu, jioni ya tarehe 28 Juni mwaka huu, kuwa Lissu amepoteza sifa za kikatiba za kuendelea kuwa mbunge. Alisema, amechukua uamuzi huo, kufuatia kutoonekana bungeni kwa muda mrefu bila yeye kuwa na taarifa ya maandishi; na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Akiongea kwa hisia kali, Spika Ndugai alisema, “Septemba 2017, kwa sababu ambazo zinafahamika kwa kila mtu, mbunge wa Singida Mashariki, aliondoka hapa nchini kwa ajili ya matibabu nchini Kenya.

“Kufanya hadithi iwe fupi, mtakumbuka zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akionekana kwenye vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa akifanya mihadhara mbalimbali.

“Lakini kwa muda wote huo, hajafika bungeni na hajawahi kuleta taarifa yeyote ile kwa Spika kuhusu mahali alipo na anaendeleaje; wala hajawahi kuleta taarifa kupitia kwa uongozi wake wa kambi au uongozi wa Bunge.”

Kufuatia hali hiyo, Ndugai alisema, Katiba ya nchi ipo wazi katika mambo ya aina hiyo, na kwamba baadhi ya wabunge wameshapata matatizo kutokana na utoro kama huo wa Lissu.

Aliongeza, “…wa (utoro) kushindwa hata kuwambia Spika niko mahala fulani naendelea na jambo fulani hivi hakuna chochote, yaani kama kum dis-regard Spika kama hakuna chochote.

“Jambo la pili, wabunge wanatakiwa kujaza taarifa zenye maelezo ya mali na madeni kama Katiba inavyotaka. Tunatakiwa tujaze fomu mbili, na nakala inabaki kwa Spika.”

Alisema, “baada ya kuona kwenye kumbukumbu zangu hakuna fomu za Lissu, nilichukua jukumu la kupata uhakika wa jambo hili kwa Kamishna wa Tume ya Maadili na nilijibiwa kwa barua kwamba Lissu hajawasilisha na hawana taarifa zozote.”

Spika Ndugai alisema, kwa maana hiyo, Lissu hakuwa amejaa fomu na kwamba katika mazingira hayo, kifungu cha 37 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka kumtaarifu mwenyekiti wa NEC kuhusu suala hilo.

“Napenda kuwafahamisha kuwa nimemwandikia mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba jimbo la Singida Mashariki lipo wazi, alijaze kwa mujibu wa sheria zetu. Nimefanya hivyo kwa sababu hizo mbili – kushindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge kwa muda mrefu bila kutoa taarifa kwa Spika na kutotoa taarifa za mahali alipo na kugoma kutoa tamko la mali na madeni kama ibara ya 71 (1g) inavyotaka,” ameeleza Ndugai.

Lissu amekuwa nchini Ubelgiji kwa matibabu ya majeraha yaliyotokana na shambulio la risasi, tokea tarehe 6 Januari 2018. Shambulizi dhidi ya Lissu, lilifanyika nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma, tarehe 7 Septemba 2017 na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika.”

Alikuwa akirejea nyumbani kutokea kwenye ukumbi wa Bunge, ambako alishiriki mjadala wa asubuhi.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa mbali na kunyimwa barua za kuvuliwa ubunge na kutopatiwa nakala ya gazeti la serikali, Lissu na kaka yake Alute, wameshindwa kupatiwa barua ya Spika kwenda kwa Kamishena wa Tume ya Maadili.

Taarifa kutoka ndani ya ofisi ya katibu wa Bunge na Spika na ambazo zimethibitihwa na Lissu mwenyewe zinasema, mwanasiasa huyo ambaye pia ni wakili wa mahakama kuu, aliandika barua kadhaa kwa Bunge kuomba nakala ya maamuzi yaliyofikiwa dhidi yake.

Hata hivyo, hadi anakwenda mahakamani kufungua shauri la kupinga kuvuliwa ubunge wake, siyo katibu wa Bunge, Steven Kigaigai wala Spika Ndugai, waliojibu barua zake.

Mtoa taarifa wetu anasema, “siyo tu kwamba hakupewa nafasi ya kujieleza, hata taarifa ya kuvuliwa ubunge wake hakupatiwa na Spika. Hakupatiwa barua iliyokwenda tume ya uchaguzi, wala barua iliyokwenda kwa Kamishna wa Tume ya Maadili; na au iliyojibiwa na tume hiyo kwa Spika.”

Taarifa nyingine zinasema, watu kaadha waliotumwa na Lissu mwenyewe na wengine na kaka yake, kufuatilia nakala ya gazeti la serikali kwa mchapaji mkuu wa serikali, lakini hawakuweza kupatiwa.

“Mara zote hizo, ndugu zetu hawa waliambiwa mara ofisi za mchapaji mkuu wa serikkali zimehamia Dodoma na hivyo magazeti hayo wanaweza kuyapata huko. Lakini hata walipokwenda Dodoma hawakuweza kuyapata. Waliambiwa magazeti yalichapishwa machache na hivyo yameisha,” ameeleza.

Katika shauri lake alilolifungua kwa njia ya Judicial Review – mapitio ya maamuzi yaliyofikiwa – Tundu Antipas Lissu, anaiomba Mahakama Kuu, imruhusu kufungua shauri la kupinga kuvuliwa ubunge wake.

Mleta maombi – Alute Mughwai – kwa niaba ya ndugu yake, anaiomba Mahakama Kuu isikilize maombi hayo ya awali na hatimaye imruhusu kufungua shauri la msingi, ili iweze kupata nafasi ya kuangalia uhalali wa maamuzi ya Spika Ndugai ya kumvua ubunge.

Alute anaiomba mahakama kumlazimisha Spika Ndugai, kumkabidhi nyaraka zote zinazohitajika, ikiwamo barua ya kumvua ubunge Lissu na barua yake aliyomuandikia mwenyekiti wa NEC kumjulisha kuwa jimbo la Singida Mashariki, limekuwa wazi.

Anaiomba pia mahakama itoe amri ya muda ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo la Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu na baada ya kumaliza kusikiliza shauri hilo, mahakama itengue na kutupilia mbali maamuzi ya Ndugai.

Alute ameeeleza katika hati yake ya kiapo historia mzima ya shambulizi dhidi ya ndugu yake, kuondoka kwake nchini kwa ajili ya matibabu na kusisitiza, “viongozi wote wa Bunge na Serikali, wanafahamu na  waliomtembelea akiwa kwenye matibabu jijini Nairobi, nchini Kenya na Ubelgiji.”

Katika maelezo yake, Alute anasema, Spika wa Bunge wakati akichukua uamuzi wa kumvua ubunge, hakumpa sababu za kufanya hivyo na kwamba Lissu alihukumiwa bila kupewa haki ya kusikilizwa.

Kuhusu madai ya kushindwa kuwasilisha tamko kuhusu mali na madeni, Alute anasema, Lissu alikuwa katika matibabu hospitalini nje ya nchi na kwamba spika alikuwa anatambua na au alipaswa kutambua hivyo kuwa alijeruhiwa vibaya wakati wa mapumziko ya vikao vya Bunge.

Anasisitiza kuwa katika muda wa miaka saba ya utumishi wake kama mbunge, alitekeleza wajibu wake kama mbunge; alitekeleza wajibu na majukumu yake kikamilifu kwa kuhudhuria vikao na kushiriki katika mijadala mbalimbalki ndani ya Bunge.

Anaiomba mahakama isikilize na kutoa maamuzi ya maombi yake haraka, vinginevyo Mtaturu ataapishwa kushika wadhifa huo.

Anasema, hatua yoyote ya kutosikiliza shauri lake kwa haraka, litamuathiri moja kwa moja kwa kuwa amepoteza haki zake zote, kinga na msilahi yake yanayoambatana na wadhifa wake wa ubunge.

Mtaturu alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Singida Mashariki (DED), kuwa mbunge halali wa jimbo hilo, tarehe 19 Julai 19 mwaka huu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Mataifa Afrika Mashariki yawasilisha bajeti 2024/2025 inayolenga kukuza uchumi

Spread the loveMataifa manne ya Afrika Mashariki jana Alhamisi yamewasilisha bungeni bajeti...

Habari za SiasaTangulizi

Gesi asilia, petroli kodi juu

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye...

Habari za SiasaTangulizi

Bilioni 155.4 kugharamia kicheko cha wastaafu 2022-2030

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema jumla ya Sh...

error: Content is protected !!