April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mambo matano Bunge jipya

Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spread the love

WAKATI Bunge la 12 likianza shughuli zake Jumanne tarehe 10 Novemba 2020 jijini Dodoma, mambo matano yanatarajiwa kujili ndani ya Bunge hilo ambalo limesheheni wabunge wengi kutoka chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Utaratibu wa mkutano wa kwanza wa Bunge unatawaliwa na Kanuni namba 22 hadi 26 za Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari, 2016 zinazozungumzia mikutano na vikao vya Bunge.

Kanuni ya 22 (1) na (2) inaeleza mkutano wa kwanza wa Bunge jipya utafanyika mahali, tarehe na saa ambayo Rais atatamka wakati akiitisha mkutano huo na kwamba mkutano huo utaendelea kwa muda wowote ambao utahitajika kwa ajili ya kutekeleza na kukamilisha shughuli zilizopangwa katika mkutano huo wa kwanza.

Tarehe 5 Novemba 2020, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, alitangaza kuliitisha Bunge hilo jipya litakaloanza kikao cha kwanza Jumanne ya tarehe 10 Novemba 2020 jijini Dodoma.

Tayari Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ametangaza usajili wa wabunge wateule umeanza jana Jumamosi tarehe 7 Novemba 2020.

Steven Kigaigai, Katibu wa Bunge

Kagaigai amewataka, wabunge wateule wote wanapaswa kufika wakiwa na nyaraka; hati ya kuchaguliwa/kuteuliwa kuwa mbunge na nakala ya kitambulisho cha Taifa.

Pia, Kadi ya Benki yenye namba ya akaunti ya mbunge; cheti cha ndoa kinachotambuliwa na Serikali (kwa wenye ndoa), cheti cha kuzaliwa cha watoto wenye umri chini ya miaka 18 (kwa wenye watoto), vyeti vya elimu/taaluma, nakala ya wasifu wa mbunge na picha (pasipoti size) nakala nane.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejikusanyia zaidi ya majimbo 255 kati ya 264. Kati ya majimbo 214 ya Tanzania Bara, CCM imeshinda 212 huku upinzani kwa maana Chadema na CUF jimbo mojamoja.

Kwa ujumla Kanuni za Bunge zinaweka wazi mambo matano makubwa ambayo yatafanyiwa kazi katika mkutano wa kwanza wa Bunge la 12.

Shughuli za Bunge (Kanuni ya 23)

Kanuni ya 23 (1) inataja shughuli za mkutano wa kwanza wa Bunge jipya kuwa ni; Kusomwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, Uchaguzi wa Spika, Kiapo cha Spika, Wimbo wa Taifa na Dua.

bunge la tanzania

Kadhalika kutakuwa na; kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, hoja ya kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika, ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Tanzania, hoja ya kujadili hotuba ya Rais na shughuli yoyote ambayo Bunge litaona inafaa kushughulikiwa kwa wakati huo.

Kifungu cha 2 cha kanuni ya 23 kinaeleza, mwanzoni mwa kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya, Katibu atasoma Tangazo la Rais la kuitisha Bunge jipya.

Uchaguzi wa Spika

Kanuni ya 23 (3) inasema, baada ya Tangazo la Rais kusomwa, kikao kitajigeuza kuwa mkutano wa uchaguzi wa Spika na kifungu cha 4 kinaeleza, Katibu wa Bunge atamwomba mbunge asiye mgombea wa nafasi hiyo ya Spika kutoka miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa bungeni mfululizo kwa muda mrefu awe mwenyekiti wa mkutano huo wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, baadhi ya wabunge wenye sifa ya kuwa mwenyekiti waliokaa bungeni muda mrefu mfululizo na majimbo yao kwenye mabano ni; Mussa Zungu (Ilala), William Lukuvi (Ismani) na Jenista Mhagama wa Peramiho.

Job Ndugai

Katika kifungu cha 5 cha kanuni hiyo ya 23, kinasema, Katibu wa Bunge atagawa karatasi za kura kwa wabunge na uchaguzi wa Spika utafanywa kwa kuzingatia utaratibu wa kikanuni na baada ya uchaguzi na mshindi kutangazwa, mwenyekiti atasitisha mkutano wa uchaguzi na kutaja muda ambao Spika Mteule ataapishwa.

Spika huapishwa na Katibu wa Bunge na kifungu cha saba cha kanuni hiyo kinasema baada ya Spika Mteule kuapishwa atakalia kiti chake na kutoa hotuba fupi ya shukrani, kisha ataliahirisha Bunge hadi wakati mwingine atakaoutaja, ambapo shughuli za kuapisha wabunge wote kiapo cha utii zitaanza.

Kanuni ya 9 kifungu cha 20 kinasema kinazungumza mtu au mbunge yeyote aliyechaguliwa kuwa Spika, kabla ya kushika madaraka yake, ataapa mbele ya Bunge Kiapo cha Utii na Kiapo cha Spika.

Kiapo cha Utii;

“Mimi, ………………. naapa kwamba, nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba ya Tanzania kwa mujibu wa Sheria iliyowekwa. Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie.”

Kiapo cha Spika;

“Mimi,…………., naapa kwamba, nitaitumikia vyema na kwa moyo thabiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi zangu kama Spika wa Bunge, na katika kutimiza wajibu wa cheo hicho nitawatendea haki watu wote kwa mujibu wa Katiba, Kanuni za Bunge na Sheria, Mila na Desturi za Jamhuri ya Muungano na kwa vyovyote vile sitatoa siri za Bunge. Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie.”

Kiapo cha wabunge (Kanuni ya 24)

Katika kanuni ya Bunge ya 24, kifungu cha 1 kinaeleza kila mbunge ataapa “Kiapo cha Utii” kitakachokuwa na maneno yafuatayo:

“Mimi,…naapa kwamba, nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyowekwa. Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie.”

Wakati mbunge akiapa, kifungu cha 2 kinaeleza, mbunge anayeamini kuwa kuna Mungu, atalazimika kushika Biblia au Kurani au kitabu kingine kitakatifu kinachotambuliwa na imani ya dini yake.

Taarifa ya Rais (Kanuni ya 25)

Baada ya shughuli ya kuwaapisha wabunge kukamilika, kanuni ya 25(1) – (4) inaeleza Spika atasoma taarifa ya Rais inayotaja jina la mbunge anayempendekeza kuwa Waziri Mkuu ili aweze kuthibitishwa na Bunge.

Baada ya Spika kutaja jina la mbunge anayependekezwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atatoa hoja ya kuliomba Bunge lithibitishe uteuzi wa mbunge husika kuwa Waziri Mkuu.

Mara baada ya kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, Bunge litamchagua Naibu Spika na iwapo Bunge litakataa kumthibitisha Waziri Mkuu, Spika atamjulisha Rais kuhusu uamuzi huo.

Kanuni ya 26 (1) inasema baada ya uchaguzi wa Naibu Spika, Spika atalitangazia Bunge mahali, siku na muda ambao Rais atalihutubia na kulifungua rasmi Bunge jipya. Baada ya tangazo hilo, Spika anaweza kuahirisha shughuli za Bunge hadi wakati huo au kuahirisha kikao cha Bunge hadi siku na muda atakaoutaja.

Ufunguzi wa Bunge (Kanuni ya 26)

Kanuni ya 26 (2) inazungumzia siku ambayo Rais atalihutubitia Bunge pamoja na kufanya uzinduzi wake, kwamba mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge, atapokewa na Spika akifuatana na Waziri Mkuu na kisha atakaribishwa ili alihutubie na kulifungua rasmi Bunge jipya.

Mara baada ya hotuba ya Rais, Waziri Mkuu atatoa hoja ya kuahirisha Bunge hadi mahali, siku na muda atakaoutaja.d

error: Content is protected !!